×

Makambo Mali Ya Yanga, Gsm Yamaliza Mchezo DR Congo

YANGA wanatamani kuona mshambuliaji wao kipenzi, Heritier Makambo, anarejea katika klabu hiyo lakini bado kidogo tu staa huyo atakabidhiwa jezi yake yenye rangi ya njano na kijani, hiyo ni baada ya Kampuni ya GSM kumalizana na mchezaji huyo fasta.

 

Makambo ambaye ni raia wa DR Congo, ni kati ya wachezaji waliopo kwenye orodha ya nyota wanaowahitaji katika kuiimarisha safu ya ushambuliaji inayoundwa na Yikpe Gnaimen, David Molinga, Tariq Seif na Ditram Nchimbi.

 

Makambo ambaye wakati anatua Yanga hakuwa akiaminika kama anaweza kufanya makubwa lakini aliwakosoa wote waliokuwa wakimbeza, hiyo ni baada ya kufunga mabao 17 msimu wa 2018/19 na kumaliza wa tatu nyuma ya Meddie Kagere ambaye alikuwa kinara na mabao yake 23, wa pili alikuwa Salim Aiyee (18).

Baada ya msimu huo kumalizika, Makambo alisepa zake na kwenda Horoya Athletic Club inayoshiriki Ligi Kuu ya Guinea kwa dau la zaidi ya shilingi milioni 200, msimu huu amecheza mechi nane na kufunga bao moja katika ligi na amekuwa hapati nafasi ya kuanza mara kwa mara kama alivyokuwa Yanga.

 

Kwa mujibu wa chanzo kutoka ndani ya Yanga, mabosi wa GSM tayari wameshamalizana na Makambo kila kitu ambaye yuko kwao DR Congo kwa mapumziko na kinachosubiriwa ni kwenda kuzungumza na Horoya pekee.

 

“Mabosi wa Yanga wamemalizana na mshambuliaji Makambo ambaye yupo kwao DR Congo kwa mapumziko ya mwezi huu mmoja baada ya ligi zote kusimamishwa kutokana na Corona.

 

“Tayari makubaliano ya awali yamefanyika na huenda usajili wa Makambo ukawa miongoni mwa sajili za kwanza kwa klabu ya Yanga katika msimu ujao wa ligi.

 

“Yanga siku chache zilizopita ilimtuma kiongozi wake wa Kamati ya Utendaji nchini DR Congo ambao walikutana na kuzungumza na meneja wa mshambuliaji huyo ambaye yeye atakwenda kumalizana na Horoya kabla ya kuja nchini kusaini mkataba,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Aidha Championi lilizungumza na mmoja wa mawakala wa wachezaji Afrika ambaye anatambulika na Shirikisho la Soka la Kimataifa, ambaye alisema dau la Makambo linafikia kiasi cha dola 300,000 (Sh Mil 689.6).

 

Championi Jumamosi lilimtafuta Msemaji na Ofisa Mhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz, kujua kuhusu usajili huyo ambapo alisema: “Kuhusu Makambo bado haijawa taarifa rasmi ingawa dau hilo linaonyesha kuwa Makambo na Horoya watanufaika kutokana na hela hiyo ya usajili, lakini ngoja tusubiri wakati wa usajili ukifika tutalizungumza zaidi.”

Stori: Wilbert Molandi na Abdulghafal Ally

Leave a Comment