Rais wa Malawi na mawaziri wote nchini humo watakatwa asilimia kumi ya mishahara yao ya miezi mitatu ili kupata fedha za kukabiliana na mlipuko wa virusi vya corona.
Rais Peter Mutharika alitangaza hatua hiyo ili kukabiliana na athari za kiuchumi ambazo zimesababishwa na corona.
Malawi imeripoti kisa cha kwanza cha mgonjwa mwenye virusi vya corona siku ya Alhamisi, na lilikuwa taifa la mwisho kutangaza kuwa na maambukizi.
Hatua hii imechukuliwa wakati rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta alitangaza kwamba yeye na makamu wake watapunguziwa asilimia 20% katika mshahara wao.
Alihimiza hatua hiyo ichukuliwe na viongozi wengine serikalini kukatwa 10%.
Bwana Kenyatta na wabunge wa Kenya ni miongoni mwa watu wanaolipwa fedha ningi zaidi barani Afrika.
