×

Breaking: Wagonjwa wa Corona Tanzania Wafikia 24

WAZIRI wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu, ametangaza uwepo wa wagonjwa wengine wapya wanne wa maambukizi ya virusi vya corona nchini humo.

 

Ametangaza leo Jumatatu Aprili 06, 2020 katika taarifa yake kwa vyombo vya habari inayoelezea mwenendo wa hali ya corona nchini kuwa kati ya wagonjwa hao wanne, wawili wanatoka Tanzania Bara na wawili wanatoka Zanzibar.

 

“Wizara ya Afya imethibitisha kuwepo kwa kesi mpya nne za maambukizi ya virusi vya corona wanaosababisha ugonjwa wa Covid-19, V zilizopatikana Dar es Salaam, Mwanza na Zanzibar na kufanya kuwepo kwa jumla ya kesi 24 zilizoripotiwa tangu kuanza kwa ugonjwa huu nchini,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

 

Amesema kuwa wagonjwa hao wapya ni pamoja na wawili ambao walitolewa taarifa na waziri wa afya Zanzibar jana Jumapili.

 

Taarifa hiyo imesema kuwa wagonjwa wawili wa Tanzania Bara wote ni wafanyabiashara na ni raia wa Tanzania ambapo mmoja ni mkazi wa Mwanza aliyewasili kutoka Dubai Machi 24 na mwingine mkazi wa Dar es Salaam.

 

Imesema pia kuwa wagonjwa wote wako chini ya uangalizi wa wataalam wa afya katika vituo maalum vya tiba vya Dar es Salaam, Mwanza na Zanzibar huku wizara ikiendelea kuwafuatilia watu wa karibu waliowahi kukutana na  wagonjwa hao.

 

“Wagonjwa wawili wapya wa corona Tanzania Bara wote ni Watanzania ambapo mmoja ni mwanaume (41) mkazi wa Mwanza aliyeingia nchini kutoka Dubai kupitia uanja wa ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam na kuelekea Mwanza na mwingine ni mwanaume (35) mfanyabiashara, wote wapo chini ya uangalizi wa watoa huduma.

 

“Serikali inatoa msisitizo kwa wananchi kuzingatia maelekezo ya wataalam wa afya ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona hususani kwa kunawa mikono kwa maji yanayotiririka na sabuni, kuepuka mikusanyiko isiyo lazima na kukaa umbali wa mita moja kati mtu na mtu,” amesema.

Leave a Comment