WAZIRI Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson, amelazwa hospitalini ili kufanyiwa vipimo vya virusi vya corona, siku kumi baada ya kukutwa na virusi vya ugonjwa huo, ofisi yake ya Downing Street imesema.
Alikimbizwa katika hospitali moja ya mjini London siku ya Jumapili akionyesha dalili za virusi hivyo ikiwemo kiwango cha juu cha joto mwilini. Imedaiwa kuwa hatua hiyo ya tahadhari ilichukuliwa kutokana na ushauri wa daktari wake.
Waziri mkuu bado ndiye msimamizi wa serikali, lakini waziri wa masuala ya kigeni nchini humo anatarajiwa kuongoza mkutano kuhusu virusi vya corona siku ya Jumatatu.
Hatua hiyo inajiri baada ya Malkia Elizabeth kulihutubia taifa akisema kwamba Uingereza itafanikiwa katika vita vyake dhidi ya mlipuko wa virusi hivyo.
Katika hotuba isiyo ya kawaida, mfalme huyo aliwashukuru raia kwa kufuata maelezo ya serikali kusalia nyumbani huku akiwapongeza wale waliojitolea kuwasaidia wengine.
Pia aliwashukuru wafanyakazi muhimu akisema kuwa kila saa la kazi linazidi kuirejesha Uingereza katika hali yake ya kawaida.
Hotuba hiyo inajiri huku idadi ya watu waliofariki kutokana na virusi hivyo nchini Uingereza ikipanda na kufikia 4,934.
Akizungumza katika jumba la kifalme la Windsor, malkia huyo alisema kwamba wamekumbwa na changamoto nyingi katika siku za nyuma lakini hii ni tofauti.
Aliongezea kwamba wakati huu wataungana na mataifa mengine duniani kwa kutumia hatua za kisayansi ili kujiponya. na watafanikiwa na kwamba ufanisi huo utakuwa wa kila mtu.
