LICHA ya kwamba mchezo wa kuogelea ni mojawapo ya michezo inayosadikika kuanza mwaka 1800 huko barani Ulaya, bado ni mchezo ambao haujapewa kipaumbele kama mojawapo ya michezo muhimu hapa nchini.
Hali hiyo inatokana na hamasa duni, pamoja na kudorora kwa washiriki wa Tanzania katika mishindani ya mchezo huo ambao kwa mara ya kwanza ilianza kwenye michezo ya Olimpiki ilifanyika 1896 mjini Athens Ugiriki.
Hata hivyo, pamoja na mapitio hayo, wapo vijana wachache au watoto ambao wameanza kuonesha mwanga kuelekea katika mashindano makubwa ya mchezo huo katika miaka ijayo.
Mmoja wa watoto hao ni Romeo Mihaly Asubisye (12) anayesoma kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Genesis iliyopo Dar es salaam.
Romeo ambaye alizaliwa mkoani Arusha, alianza kufundishwa kuogelea akiwa na umri wa miezi sita na mama yake aitwaye Amina Mohamed.
Alipofikisha miaka minne alianza mafunzo rasmi kutoka kwa makocha wenye uwezo na viwango bora dunaini.
Akizungumza na gazeti hii Romeo anasema anapenda kuogelea na ndoto yake kubwa pindi atakapotimiza umri wa miaka 16 na kuendelea ni kushiriki katika mashindano ya Olimpiki na kuibuka na medali.
REKODI ALIZOWEKA
Anasema mwaka 2015 akiwa na miaka nane alishinda medali ya dhahabu kwenye mbio za mita 50 kwa free style na mita 50 breast stroke.
“Yalikua ni mashindano ya klabu za Swim fast na Swim club kutoka Florida Marekani ambapo nilishinda na kuwa mshindi wa jumla.
“Mwaka 2016 nikiwa na miaka tisa nilishiriki Mashindano ya Tanzania National Club Championship na kushinda medali tano za dhahabu, mbili za silva na moja ya shaba katika mashindano ya first run up kwa umri wa miaka tisa,” anasema.
Anasema mwaka 2017 alikua mshindi wa jumla kwa kushinda medali za dhahabu nane katika mashindano ya Tanzania National Club Championship.
“Mwaka 2018 nilivunja rekodi na kushinda medali za dhahabu nane na kuwa mshindi wa jumla katika mashindano yaliyojumuisha vijana wenye umri wa miaka 10-11 katika mashindano ya Tanzania Junior Club Championship.
“Mwaka 2019 katika mashindano ya Cana Zone Three Africa yaliyofanyika nchini Kenya vilevile nilishinda medali tisa za dhahabu na kuwa mshindi wa jumla,” anasema.
Anasema katika mashindano hayo timu kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Sudan, Malawi, Rwanda, Uganda, Burundi na Zambia zilishiriki.
Aidha, mwaka 2019 katika mashindano ya Tanzania National Clay Championship alishinda medali za dhahabu tisa akiwa na miaka 12.
Anaongeza kuwa Januari mwaka huu katika mashindano ya Morogoro Invitation Gala alikuwa mshindi wa jumla kwa kushinda medali za dhahabu nane.
“Februari 22 mwaka huu katika mashindano ya Tallis Invitation Gala yaliyofanyika IST (International School of Tanganyika) pia nilikuwa mshindi wa jumla kwa kushinda medali za dhahabu nane.
WITO KWA SERIKALI
Aidha, anasema mojawapo ya changamoto anayokumbana nayo kwa sasa ni uhaba wa maeneo ya kuogelea.
“Kwa sababu kuna pool moja tu lililopo pale IST ndio tunalotumia wanamichezo wote, naiomba serikali ituangalie pia na sisi wanamichezo ya kuogelea kwa sababu ni michezo mizuri yenye fursa kama michezo mingine,” anasema.
Aidha, anatoa wito kwa wazazi kuwapa nafasi watoto wao kushiriki michezo ya kuogelea kwa sababu ni mojawapo ya michezo ambayo inawajenga kimwili, kiakili na hata kuwa na matokeo mazuri darasani.
NA MWANDISHI WETU






