BAADA ya hivi karibuni kudaiwa kufumaniwa na mrembo mwenye umbo matata Bongo, Nicole Joyberry Mbaga, staa wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’ au ‘Harmo’ na mchumba’ke wa muda mrefu, Sarah Michelloti, moto umewaka ile mbaya, IJUMAA WIKIENDA linakupa habari kamili. Kwa mujibu wa vyanzo vya ndani, Sarah ambaye ni raia wa Italia ana hasira mno dhidi ya Harmo kutokana na kitendo hicho cha kumfumania.
Katikati ya hasira hizo, inadaiwa kuwa, Sarah amejikuta akimpandisha presha mama mzazi wa Harmo, Habiba Chivalavala baada ya kudaiwa kumfokea kama mtoto mdogo alipomtembelea nyumbani kwake, Mbezi-Beach jijini Dar mwishoni mwa wiki iliyopita.
Chanzo hicho cha habari kiliendelea kusema kuwa, mama wa Harmo yalimkuta hayo baada ya kutoka kijijini kwao, Chitoholi mkoani Mtwara hadi Dar ambapo huwa anafanya biashara ya kuku na hufika nyumbani hapo kwa mwanaye kumsalimia.
Inadaiwa kuwa, safari hii ilikuwa tofauti kwani alipotinga nyumbani hapo akiwa amebeba na zawadi ya kuku wawili wa kienyeji kwa ajili ya mwanaye, mambo hayakwenda sawa kwa sababu Sarah alimfokea kama mtoto mdogo kwa kile alichodai kuwa, amekwenda bila taarifa.
“Hii siyo mara ya kwanza kwa mama wa Harmo kukutana na kisirani cha Sarah kwani alishakutana nacho mara kibao, lakini huwa anamvumilia tu mkwe wake huyo,” kilidai chanzo hicho.
SARAH AGEUKIA MITUNGI
Chanzo hicho kiliendelea kueleza kuwa, kwa sasa Sarah hayupo sawa kutokana na kuyumba kwa uhusiano wake na Harmo hivyo amekuwa akipiga mitungi kwa sana, yaani analewa na kuonesha tabia za ukorofi.
HARMO AGOMA KUREJEA NYUMBANI
Kwa upande wa Harmo naye anadaiwa hayupo vizuri na hana furaha kabisa na Sarah ambaye inasemekana ndiye muwezeshaji wake kifedha. Inasemekana kwamba, baada ya Sarah kumfokea mama mkwe wake huyo, Harmo hakurejea nyumbani siku hiyo hali iliyomsababisha Sarah kwenda kufanya fujo kwa mrembo aliyedaiwa kufumaniwa na mpenzi wake huyo, Nicole kwa madai kuwa, jamaa huyo alilala huko.
NI KIKI?
Baadhi ya wadau wa burudani wanadai kuwa, sarakasi za Harmo na Sarah zinaibua hisia kuwa huwenda wanafanya hivyo kama sehemu ya kiki ya kuitangaza albam ya mwanamuziki huyo aliyoutoa hivi karibuni inayokwenda kwa jina la Afro East.
Hata hivyo, Sarah alionekana kumuondoa Harmo kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram kama mmoja wa wafuasi wake.
MENEJA ANASEMAJE?
Ili kuujua ukweli wa yanayoendelea, Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lilimtafuta meneja wa Harmo, Beauty Mmari ‘Mjerumani’ ambaye alisema hawezi kuzungumza kwa kuwa ni mambo binafsi. “Kuhusu hayo yanayoendelea kwa Harmo na Sarah siwezi kuzungumzia maana ni maisha yao binafsi, mimi ninazungumza kuhusu kazi zake tu,” alisema Beauty.
