×

Makapu: Eymael Amenifanya Niwe Katili Uwanjani

BEKI wa Yanga, Said Juma Makapu, amesema kuwa kocha Luc Eymael amekuwa akimpatia mbinu zinazomfanya awe katili uwanjani na kucheza michezo mingi bila presha wala woga.

 

Makapu amefunguka kuwa, tangu Eymael achukue jukumu la kuinoa timu hiyo msimu huu, amekuwa akipewa nafasi kubwa ya kuanza kikosi cha kwanza na kutengeneza muunganiko mzuri sehemu ya ulinzi pamoja na Lamine Moro, huku akipewa mbinu na mikakati mipya ya kucheza mechi kubwa na ndogo bila woga wowote.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Makapu alisema amefundishwa na makocha wengi ndani ya kikosi hicho tangu alipojiunga na Yanga lakini Eymael ndiye mwalimu anayempatia uhuru wa kucheza na kujiamini, huku akimpandikiza roho ya ukatili anapokuwa uwanjani hali inayomsaidia kutimiza majukumu yake vizuri.

 

“Eymael ndiye kocha pekee aliyenipandikiza roho ya ukatili na kujiamini pindi ninapokuwa uwanjani, tangu nijiunge na Yanga naweza kusema huyu ndiye kocha wa kwanza ambaye amenibadilisha kimbinu na kiakili na ndiyo maana kwa sasa nimekuwa nikipewa nafasi ya kucheza kwa kuwa nimekuwa nikitimiza majukumu yangu bila woga wala presha,” alisema Makapu.

 

Makapu tangu ajiunge na kikosi hicho, amefundishwa na makocha wengi, akiwemo Marcio Maximo, Hans van Der Pluijm, George Lwandamina na Mwinyi Zahera lakini wote hao walikuwa wanamuweka zaidi benchi.

Issa Liponda, Dar es Salaam

Leave a Comment