×

Vitalis Mayanga Afunguka Kisa Cha Kuhisiwa Kuihujumu KMC

“NAKUMBUKA mchezo wangu wa mwisho kuichezea KMC ilikuwa dhidi ya Kagera Sugar ambapo tulipoteza kwa mabao 2-1, kwa kuwa nilionekana kukosa nafasi za wazi, basi nikahisiwa kuwa nilikuwa naihujumu timu, nikasimamishwa kucheza na baadaye kupewa barua ya kuachwa kabisa,” anaanza kueleza mshambuliaji wa klabu ya soka ya Ndanda Vitalis Mayanga.

 

Mayanga aliuanza msimu huu akiwa KMC lakini majeraha na kukosa nafasi, vilisababisha aishie benchi muda mwingi kabla ya kuhamia Ndanda katika dirisha dogo.

 

Alipotua Ndanda tu, Vitalis akageuka kuwa lulu na kufanikiwa kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Machi kabla ligi haijasimamishwa na Corona, leo hii Championi Jumatatu limemtafuta Mayanga aliyezaliwa Aprili 14, 1999 mkoani Kagera na kupiga naye stori kama ifuatavyo;

 

NINI SIRI YA KUZOEA MAZINGIRA KWA URAHISI NDANDA?

“Kwangu Ndanda ni nyumbani kwani nilishawahi kuwa hapa kipindi nikiwa chini ya kocha Malale Hamsini, hivyo hayakuwa mazingira mapya kwangu lakini pia nashukuru kwani nimepata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa viongozi na wachezaji wenzangu.

“Lakini pia mpaka nisajiliwe katika dirisha dogo, ilimaanisha kuwa waliniamini naweza kuja kuisaidia timu, hivyo hata mimi nilikuja hapa nikiwa nimejiandaa.

 

MKATABA WAKO NA NDANDA UKOJE?

“Watu wengi wanajua mimi niko hapa kwa mkopo kutoka KMC lakini ukweli ni kuwa mkataba wangu na KMC ulikuwa mwishoni hivyo KMC waliniacha kwa barua ya ruhusa.

“Na hapa Ndanda nimesaini mkataba wa miezi mitano ambao utaisha mwishoni mwa msimu huu.

Kwa nini KMC ilikuwa haifanyi vizuri kwenye ligi?

 

“Hata sisi wachezaji tulikuwa tunashangaa kwani katika timu za ligi kuu ambazo zilikuwa zinafanya mazoezi ya nguvu ambayo hata sijawahi kufanya kwenye timu nyingine, ni pamoja na KMC, kwani tulikuwa tunacheza vizuri lakini kukawa na tatizo la kutofunga mabao, nafikiri tatizo lilikuwa hapo.

 

VIPI KUSUHU WEWE KUSIMAMISHWA KWAMBA UNAIHUJUMU KMC?

“Mimi sijasema kwamba wamenisimamisha kwamba nilikuwa nahujumu timu, bali kuna maneno ambayo yalipelekwa kwa viongozi wangu wa juu, ndiyo nikasimamishwa kucheza KMC na baadaye uongozi uliona siyo busara mimi kukaa bila kucheza wakati nina mkataba nao, wakaamua kunipeleka Ndanda.

 

NDANDA INAWEZAJE KUFANYA VIZURI LICHA YA CHANGAMOTO ZA KIUCHUMI?

“Ninachoweza kujivunia kuhusu Ndanda ni kuwa kila mtu anajua wajibu wake na ndiyo maana licha ya klabu kuwa katika hali mbaya ya kiuchumi, bado unaweza kuona wachezaji wanajituma.

“Ukija mazoezini unaweza kushangaa jinsi watu wanavyopambana kila mtu huamua kusahau ugumu alionao na kupambana kwa ajili ya timu.

 

“Lakini hata viongozi hujitahidi kufanya malipo licha ya kwamba yanaweza kuchelewa ila unaona kabisa wanavyopambana kuhakikisha kidogo kinachopatikana wanalipa.

UNAFANYA NINI KIPINDI HIKI LIGI IKIWA IMESIMAMA?

“Kwa sasa natumia muda wangu mwingi kukaa na familia yangu (mke na mtoto mmoja).

 

BEKI GANI KWAKO NI BORA ZAIDI NDANI YA VPL?

“Mabeki wote ambao nimewahi kukutana nao ni wakali ila kama utaniambia nimchague mmoja, basi nitamtaja beki wa KMC, Abdallah Mfuko.

 

TUKIO GANI LA UWANJANI HUWEZI KULISAHAU?

“Sitasahau tukio la Polisi Tanzania kupewa goli la mpira wa ‘fair play’ (mchezo wa kiungwana) katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Ushirika pale Moshi.

 

“Ishu yenyewe ilikuwa hivi; sisi tulikuwa tukishambulia kuelekea goli la Polisi lakini mchezo ukasimamishwa ili mchezaji wao apate kuhudumiwa, cha kushangaza baada ya mchezaji wao kutolewa, Polisi walianza mpira kama kawaida wakati sisi tukijua wanatoa ‘fairplay’.

 

“Sasa katika sekeseke la kuchukua mpira mchezaji wao Mateo Anthony akaangushwa na mwamuzi akaamuru iwe penalti.

“Baada ya hapo kama dakika tatu na mimi nikasawazisha ila goli langu likakataliwa na katika kulalamika nikapewa kadi ya njano, dah hiyo ishu ilinitoa mchezoni kabisa yaani.

 

NINI HUWEZI KUKISAHAU KABISA MAISHANI?

“Kitu ambacho siwezi kusahau ni pale Stand United ilipotaka kuniharibia maisha yangu ya soka kabisa, nakumbuka msimu wa 2017/18 nilisajiliwa Stand katika dirisha la Januari.

“Kipindi hicho Stand ikiwa ya mwisho kwenye msimamo, pamoja na wenzangu tukapambana na kuinusuru Stand isishuke daraja.

 

“Baada ya hapo nikapata madili kutoka klabu za Ndanda na Geita lakini viongozi wa Stand wakaniambia kuwa niachane nazo kwa kuwa wana mpango wa kuniongezea mkataba.

 

“Lakini hadi zinabaki siku nne dirisha la usajili kufungwa hakukuwa na taratibu zozote na licha ya kunipunguzia dau la usajili na mimi kukubali lakini unaambiwa jamaa wakaja kuniambia nitafute timu saa chache kabla ya dirisha kufungwa.

 

“Ishu hiyo ilinipa wakati mgumu sana lakini nashukuru Mungu, mwalimu Malale Hamsini alinichukua na kuniunganisha katika kikosi chake cha Ndanda kabla ya dirisha kufungwa.

 

ULIIPOKEAJE TUZO YA MCHEZAJI BORA MWEZI MACHI?

“Ilikuwa tuzo muhimu sana kwangu kwani kutokana na yaliyonipata nikiwa KMC wengi waliamini basi ningepotea moja kwa moja lakini namshukuru Mungu kwa mafanikio niliyoyapata.

 

“Mafanikio haya yameonyesha wazi kumbe mimi sikuwa tatizo pale KMC na ukweli ni kwamba hata mimi sikuamini kama nimeweza kuibuka bora kati ya wachezaji karibu 600 wa Ligi Kuu Bara,” anasema Mayanga ambaye ana mabao mawili msimu huu.

JOEL THOMAS, Dar es Salaam

 

Leave a Comment