×

Majaliwa: Marufuku Sunday Schools, Madrasa – Video

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuna taarifa kuwa baada ya masomo kusitishwa kwa sababu ya Covid 19 watoto hao sasa wamekuwa wakienda makanisani na misikitini kwa ajili ya kujifunza.

 

Amesema alipokutana na maaskofu na mashehe walikubaliana kusitisha huduma nyingine zote isipokuwa ibada tu hivyo ni marufuku kwa watoto kukusanywa kwa kisingizio cha Sunday Schools na madrasa na kwamba makanisa na misikiti itumike kwa shughuli za ibada pekee za kuliombea taifa tena kwa muda mfupi na baada ya ibada waumini watawanyike mara moja.

 

“Ninazo taarifa kwamba wameanzisha mfumo wa kupeleka watoto kwenye madarasa ya dini maarufu kama Sunday Schools. Tumeruhusu ibada tu, na hizo ibada lazima ziangaliwe ziwe za muda mfupi kadri inavyowezekana. Tumesisitiza kwenye makanisa au misikiti ambako ibada zinafanyika, waumini wakae kwa kuachiana nafasi,” alisema Majaliwa jana.

 

Aliongza kwamba  changamoto inajitokeza kwenye makanisa makubwa ambayo yana waumini karibu 3,000 na kweli,  “Hayo sasa yatakuwa ni makongamano. Tunaaamini maaskofu na mufti wataliweka vizuri suala hili la sunday school na madrassa,” amesema.

 

Amesema serikali haitazuia biashara kwenye masoko, maduka au supermarkets isipokuwa amewataka wenye biashara hizo wahakikishe wanaweka ndoo za maji na sabuni ili wateja wanawe mikono kabla ya kuingia kupata huduma na wakati wanapotoka kupatiwa huduma hizo.

 

Kuhusu mikusanyiko mingine,  amesema watu wanapaswa wajizuie kwenda kuzagaa kwenye vituo vya mabasi na kama hawana shughuli za lazima za kufanya huko, basi wabakie majumbani kwao.

Leave a Comment