×

Trump Kusitisha Fedha WHO, China na Ujerumani Zanena

CHINAimeitaka Marekani kutotelekeleza jukumu lake kwa shirika la afya duniani (WHO) baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kusitisha ufadhili katika shirika hilo, akikosoa jinsi lilivyoshughulikia janga la virusi vya Corona.

 

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China, Zhao Lijian, amesema kuwa janga la virusi vya Corona limefika katika hatua ya kutisha na hivyo uamuzi wa Trump wa kusitisha ufadhili kwa WHO utaathiri mataifa yote duniani.

Rais  Trump

Marekani ndiye mfadhili mkubwa wa WHO, ikichangia zaidi ya dola milioni 400 mwaka 2019 ambayo ni asilimia 15 ya bajeti ya WHO lenye makao yake Geneva.

 

Trump ameishutumu WHO kuficha ukweli kuhusu mlipuko wa virusi vya Corona na badala yake kuamini kila taarifa iliyotolewa na China kuhusu virusi hivyo.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Heiko Maas

Hata hivyo, aliyekuwa mkuu wa idara ya ujasusi nchini Uingereza, John Sawers, amesema itakuwa bora China kubebeshwa lawama badala ya WHO.

 

Sawers amesema kuwa anafahamu hasira iliyo nayo Marekani kutokana na taarifa walizokuwa wamezificha kuhusu virusi vya Corona.

 

Na nchini Ujerumani, waziri wake wa  mambo ya nje,  Heiko Maas,  ameukosoa uamuzi wa Trump akisema kuwa kinachohitajika sasa ni kuliimarisha WHO.

Mkurugenzi mkuu wa WHO, Tedros Adhanom  (kushoto) akiwa na Rais wa China, Xi Jinping

Kupitia ukurusa wake wa Twitter, Maas ameandika:

“Lawama hazisaidii. Virusi vya Corona havijui mipaka. Tunahitajika kushirikiana katika vita hivi dhidi ya COVID-19 hasa kuimarisha shirika la WHO.”

Huku hayo yakiarifiwa, nchini Ujerumani, Ofisi ya Kansela Angela Merkel imependekeza  majimbo yote 16 ya nchi kuendelea na utekelezwaji la agizo la watu kutokaribiana hadi Mei 3 ili kuzuia kuenea kwa virusi vya Corona.

Mapendekezo hayo yatajadiliwa na baraza la mawaziri mjini Berlin baadaye hii leo.

Kuhusu maambukizi ya Corona nchini Ujerumani, Lothar Wieler ambaye ni mkuu wa taasisi ya utafiti ya Robert Koch amesema:

“Kwa sasa tuna uwezo wa kutosha katika hospitali zetu, hasa vitanda katika chumba cha wagonjwa mahututi na vifaa vya kusaidia wagonjwa kupumua.”

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kuwa huu si wakati mzuri wa kupunguza ufadhili katika shirika la afya duniani.

Kupitia taarifa iliyotolewa,  Guterres amesema kuwa si tu shirika la afya duniani bali mashirika yote ya kibinadamu yanayopambana na janga la virusi vya Corona hayafai kupunguziwa ufadhili hasa wakati huu.

Katibu mkuu huyo ametoa wito wa mshikamano baina ya jamii ya kimataifa katika vita dhidi ya janga la virusi la Corona.

Leave a Comment