×

WHO Lamshutumu Trump Kulinyima Fedha

MKUU wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tedros Adhanom Ghebreyesus, ameshutumu uamuzi wa Rais wa Marekani, Donald Trump wa kutopeleka fedha kwa shirika hilo na amewataka walimwengu kushikamana katika kukabiliana na janga la maambukizi ya virusi vya Corona yanayosababisha ugonjwa wa Covid-19.

 

“Tumesikitishwa na uamuzi wa rais wa Marekani kusimamisha ufadhili kwa WHO,” amesema katika taarifa kuhusiana na nchi hiyo ambayo hutoa asilimia 15 ya bajeti ya shirika hilo.

 

“WHO inajipanga upya kukabiliana na kujiondoa kwa Marekani ili kupata washirika wengine wa kujaza mapengo kama hayo na kuhakikisha kazi yetu inaendelea bila tatizo,” alisema Tedros.

 

Hata hivyo, Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, Nancy Pelosi, alichukizwa na uamuzi huo wa Trump akisema, “Kusimamisha ufadhili huo kwa WHO wakati liliongoza harakati dhidi ya virusi vya Corona, ni hatua ya kipuuzi.”

 

Hatua hiyo ya Trump imeshutumiwa na viongozi na taasisi nyingi duniani ambapo wanaona inachochea utengamano badala ya ushirikiano unaotakiwa sasa.

 

Leave a Comment