×

Jiji la Arusha Kufunga Maduka 400 – Video

HALMASHAURI ya jiji la Arusha imepanga kufunga maduka zaidi ya 400 ya wafanyabiashara iwapo watashidwa kulipa deni la sh. milion 262.5 linalotokana na malimbikizo ya kodi ya pango katika kipindi cha mwaka mmoja na kuikosesha mapato halmashauri hiyo.

 

Akiongea na vyombo vya habari kwa niaba ya mkurugenzi wa jiji hilo, kaimu mweka hazina wa halmashauri ya jiji la Arusha, Antony Kiwoli,  amesema kuwa maduka hayo yaliyopo eneo la Stendi Ndogo baadhi ya wafanyabiashara wameshindwa kulipa deni hilo na kuilazimu halmashauri hiyo kufikia hatua ya kufunga maduka hayo kama njia mojawapo ya kushinikiza wafanyabiashara hao kulipa madeni yao.

 

Amesema katika kipindi cha wiki mbili baada ya halmashauri hiyo kuanza operesheni ya kukusanya madeni baadhi ya wafanyabiashara hao wamekuwa na mwamko wa kulipa madeni yao ambapo kiasi cha sh. milioni 71 kiliweza kupatikana.

 

Kaimu mweka hazima huyo amebainisha kuwa kutokana na operesheni hiyo iliyoenda sanjari na kufunga maduka ya wadaiwa sugu, viongozi wa wafanyabiashara hao wamefika ofisini kwa mkurugenzi wa jiji hilo na kuomba kusitisha kuwafungia maduka yao kwa kwa makubaliano ya kulipa madeni yao ndani ya siku 14.

 

Awali mwenyekiti wa wafanyabiashara mkoa wa Arusha, Loken Masawe,  amesema kuwa kumekuwepo na mtafaruku mkubwa baada ya halmashauri hiyo kuanza zoezi la kufunga maduka hayo.

 

Masawe amesema kuwa wamelazimika kumwomba mkurugenzi huyo kusitisha zoezi hilo ili waweze kujipanga na kuwahamasisha wafanyabiashara wenzao kulipa madeni yao, jambo ambalo mkurugenzi huyo aliwakubalia na kuwapa siku 14 kuanzia sasa hadi Mei 1mwaka huu.

 

“Tumemwomba mkurugenzi wa jiji atupe muda ili tuweze kuwahamasisha wafanyabiashara waweze kulipa,  tunashukuru ametupa muda wa siku 14 na kuanzia kesho amesema hawatafunga maduka hayo,” amesema.

 

Leave a Comment