×

Corona: Sukari Yapaa, Serikali Yatoa Tamko – Video

SERIKALI imewahakikishia Watanzania kuwa hakuna upungufu wa sukari hivyo wananchi hawapaswi kuwa na wasiwasi wa aina yoyote ile.

 

Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa  ameyasema hayo jijini Dodoma jana Aprili 16,  2020, wakati akitoa ufafanuzi juu ya malalamiko ya wananchi kuhusu kupanda kwa bei ya sukari.

 

Amesema kuwa kila mwaka serikali imekuwa makini katika kutathmini mahitaji ya sukari kwa wananchi kadhalika uwezo wa viwanda vya ndani katika uzalishaji.

 

Bashungwa amesema ni kweli bei ya sukari imepanda lakini haisababishwi na upungufu wa sukari bali imesababishwa na waagizaji kushindwa kuagiza kwa wakati kutokana na ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na kirusi cha Corona.

 

Ili kukabiliana na kadhia hiyo serikali imetoa vibali vya jumla ya tani 40,000 kwa kampuni nne za wazalishaji ambapo kila kampuni imeagiza tani 10,000.

 

Amesema kuwa tayari sukari iliyokwishaingia bandarini kupitia kampuni ya Kagera Sugar ni tani 9,990 na imeanza kuzitoa bandarini tangu juzi jioni.

 

Kadhalika Aprili 24, 28 na 30 kampuni ya Mtibwa Sugar itaingiza jumla ya tani 10,000,   na kampuni ya Kilombero Sugar itaingiza tani 1,624 hivi karibuni kutoka Malawi na Msumbiji huku tani 1,800 ikiagizwa kutoka Afrika Kusini.

 

Sambamba na hayo amesema kuwa wiki ya kwanza ya mwezi Mei Kampuni ya Kilombero Sugar itaingiza tani 7,276 huku tarehe 15 Mei kampuni ya TPC itaingizatani 5,000 na  30 Mei tani 4,500 zitaingia nchini.

Ameongeza kuwa wizara inatarajiwa kuomba nyongeza ya tani 58,000 ili kukidhi mahitaji ya sukari kufikia Juni 2020.

 

Hata hivyo amesema kuwa asilimia 80 ya sukari ambapo kwa mujibu wa takwimu mahitaji ya sukari inayotumiwa majumbani ni kiasi cha tani 4,700,000 ambapo kati ya hizo tani 378,000 zinazalishwa nchini.

 

Pia amesema kuwa hiyo ni hatua kubwa kwa nchi na serikali katika mkakati wa kuimarisha uchumi wa viwanda huku wawekezaji wengi wakiendelea na mchakato wa uongezaji tija na uwezo wa uzalishaji.

 

Kadhalika wakulima wamekuwa na mtazamo mkubwa katika kuzalisha miwa kwa wingi ambayo wataipeleka katika viwanda vya kuchakata sukari na katika kipindi cha hivi karibuni serikali itafikia uwezo mkubwa wa uzalishaji hivyo kuwa na ziada ya sukari itakayouzwa nje ya nchi.

 

Leave a Comment