×

Senzo Atoa Kauli Ya Kishujaa Simba

MTENDAJI Mkuu wa Klabu ya Simba, Senzo Mazingisa, amesema kuwa timu yake haishindwi kumsajili mchezaji yeyote anayecheza katika ligi ya Tanzania labda kama hawamhitaji mchezaji huyo.

 

Simba imekuwa ikihusishwa na usajili wa baadhi ya wachezaji wanaocheza Ligi Kuu Bara kama beki wa Coastal Union, Bakari Mwamnyeto, beki wa Azam FC, Yakubu Mohammed na kiungo wa Polisi Tanzania, Baraka Majogoro.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Senzo alisema kuwa kutokana na aina ya wachezaji wanaopatikana hapa nchini, timu hiyo haishindwi kumsajili mchezaji yeyote ambaye watakuwa wakimhitaji labda kama hawana mpango na mchezaji huyo.

 

“Wachezaji wengi wanaocheza ligi ya Tanzania tunawamudu kwenye kuwasajili, hivyo kama kweli kuna mchezaji tunamtaka kumsajili na yupo kwenye mipango yetu hatutamshindwa labda asiwe kwenye mipango yetu.

 

“Wachezaji ambao wamekuwa shida ni wale wanaocheza katika timu kubwa za Afrika na wenye viwango vya daraja la juu hawa kidogo ndiyo husumbua kwa kuwa wana mahitaji mengi zaidi ya kusajiliwa tu,” alisema kiongozi huyo.

Stori: Marco Mzumbe, Dar

Leave a Comment