KOCHA Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, amemruhusu kiungo wake, Clatous Chama kujiunga na Yanga.Kauli ya Sven imekuja ikiwa ni siku chache tangu Yanga wahusishwe kumfuatilia kiungo huyo raia wa Zambia ambapo sakata lake limetinga kwenye Ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Simba inadai kwamba, Yanga imefanya mazungumzo na Chama wakati bado ana mkataba unaozidi miezi sita kitu ambacho ni kuvunja sharia.
Sheria za Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na TFF zinaruhusu mchezaji mwenye mkataba kuanzia miezi sita kushuka chini, kufanya mazungumzo na timu yoyote inayomuhitaji lakini si mwenye mkataba wa zaidi ya miezi sita.
Chama ambaye mkataba wake na Simba unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu wa 2020/21, mwenyewe amewahi kusema yupo tayari kuichezea Yanga pindi mkataba wake utakapomalizika.
Kiungo huyo aliyejiunga na Simba msimu uliopita akitokea Power Dynamos ya Zambia, licha ya Yanga kuhusishwa kumtaka, lakini baadaye viongozi wa klabu hiyo kupitia kwa Makamu Mwenyekiti, Fredrick Mwakalebela alisema kwamba walikuwa wanatania tu.
Sven ameliambia Championi Jumatano kuwa: “Kama Chama anataka kuondoka Simba na kwenda Yanga aende tu, milango ipo wazi.“Siyo kwake, hata mchezaji mwingine ndani ya kikosi cha Simba akitaka kuondoka kwa mapenzi yake aende. Akiona nafasi hamna ruhusa kuondoka.
”Katika hatua nyingine Sven alisema kuwa, Chama ni mchezaji mzuri, hivyo ana msaada mkubwa kikosini kwake kwani ni mtu ambaye hubadili matokeo muda wowote.
“Kwa kumzungumzia Chama, ni mchezaji mzuri, kwa sasa bado ni mchezaji wetu, anapokuwa uwanjani ana uwezo wa kubadili matokeo muda wowote. Amekuwa akifanya vizuri ingawa siwezi kuzuia mchezaji kuondoka,” alisema Sven raia wa Ubelgiji.
Stori na Mwandishi Wetu | Dar es Salaam

