ALIYEKUWA Mchungaji wa Kanisa la Mlima wa Moto na Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Askofu Dkt. Getrude Rwakatare, amezikwa leo Alhamisi, Aprili 23, 2020, katika viunga vya kanisa lake lililopo Mikocheni B, jijini Dar es Salaam.
Mazishi ya kiongozi huyo yamehudhuriwa na wawakilishi wachache wa familia na kusimamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mama Rwakatare alifariki dunia Aprili 20, 2020, katika hospitali ya Rabininsia jijini Dar es Salaam, alikokuwa akipatiwa matibabu, ambapo kwa mujibu wa mwanaye Mutta Rwakatare, alisema mama yao alikuwa akisumbuliwa na tatizo la moyo na presha.
Mama Rwakatare alizaliwa Desemba 31, 1950, amefariki akiwa na umri wa miaka 70. Aliwahi kuhudumu katika nafasi mbalimbali za uongozi, ikiwemo Ubunge wa Viti Maalum wa CCM (Mvomero) na Mbunge wa Kuteuliwa na Rais wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.



