×

Wabunge Waazimia Kujigawia Mil. 20 Kila Mmoja za Corona

WABUNGE nchini Uganda wameazimia kujigawia Shilingi za Uganda mil. 20 kila mmoja kama fedha ya ahueni wakati huu wa janga la coronavirus linalosababisha ugonjwa wa homa ya mapafu — Covid-19.Hatua hiyo imepingwa vikali na wananchi wakitaka fedha ielekezwe kwa wahudumu wa afya. Nchi hiyo ina wabunge zaidi ya 400.

Spika wa Bunge la Uganda, Rebecca  Kadaga, ametetea uamuzi huo akisema fedha hiyo itatumiwa na wabunge katika kuendeleza harakati dhidi ya ugonjwa huo katika majimbo yao.

Kadaga amedai kamba bonasi ya wabunge ni sehemu ya bajeti ya ziada iliyopitishwa wiki iliyopita kuupiga vita ugonjwa huo.  Fedha hiyo itasaidia kuwalipa madereva na magari ya dharura yanayosafirisha wagonjwa.

 

Hata hivyo, Jonathan Odur, bunge wa upinzani kutoka jiji la Kampala amesema fedha hiyo ya mgao ilipitishwa na wabunge kwa njia za ujanjaujanga.

 

Ameongeza kwamba wabunge walilaghaiwa na kukubali kuikata fedha hiyo kutoka katika fungu dogo la bajeti ya Covid-19 la sh. bilioni 104.

 

Hadi sasa Uganda ina wagonjwa 55 waliokumbwa na ugonjwa huo lakini hapajatokea kifo chochote.

 

Huku wafanyakazi wa afya wakikabiliwa na uhaba wa vifaa-tiba na vya kujikinga, wizara ya afya ya nchini humo imeomba kuongezewa sh. bilioni 400 ili kukabiliana na ongezeko la virusi hivyo na magonjwa mengine, lakini ilipewa theluthi moja tu ya kiwango hicho.

 

“Sh. bilioni kumi zilizotolewa kwa wabunge zinazidi kupunguza kiango kinachotakiwa katika sekta ya afya, na kama zingebidi zitolewe popote, basi zingetolewa kwa wizara ya afya,” anasema Odur.

 

Fedha hiyo inatarajiwa kulipwa kwa wabunge wiki hii, lakini Odur amesema atairudisha kama akipewa.

Leave a Comment