×

Utata Aliyemkata Kichwa Bibi Yake

 DUNIANI si mahali salama tena kwa maisha ya binadamu! Ndivyo unavyoweza kusema kufuatia utata mkubwa ambao umeibuka baada ya Eliakim James Mwakifuna (20), mkazi wa Kiwira Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya kutuhumiwa kumuua bibi yake, Junes Sankanye (65).

 

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Eliakim alidaiwa kumuua bibi yake huyo kwa kumchinja kama kuku na kutokomea na kichwa chake kusikojulikana.

 

Akisimulia mkasa huo wenye utata wa kutosha, mama mzazi wa mtuhumiwa wa mauaji hayo, Monica Bukuku alisema kuwa, siku mbili zilizopita kabla ya mauaji hayo, walikuwa na ugomvi wa kifamilia na mtuhumiwa ambapo alifanya uharibifu mkubwa nyumbani kwa kuvunja vioo vya nyumba na kupasua vyombo kisha kuondoka na kwenda kijijini Nkunga alikokuwa anaishi bibi yake.

 

Hata hivyo, mama huyo alisema alimfuata mtuhumiwa kwa bibi yake na kumtaka aondoke, jambo ambalo alikaidi na kuahidi kumkata kwa panga ambalo alikuwa amelishika mkononi.

 

Aliendelea kusema, jioni yake yeye (Monica) alirejea Kiwira, lakini mapema alfajiri alirudi tena nyumbani kwa marehemu ili kumjulia hali, lakini alipofika alikuta mlango umefungwa ambapo aligonga kwa muda mrefu bila kufunguliwa.

 

Alisema alipoona hivyo, ndipo alipowaita majirani ili kujua kilichowasibu mwanaye na mama yake.

Baadhi ya majirani walipofika hapo kisha kukuta mlango umefungwa na kutofunguliwa, waliamua kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Nkunga, Mariam Bachu Nurdin ambapo walivunja na kubaini bibi huyo ameuawa kisha kufunikwa na nguo zake chumbani na muuaji kutokomea na kichwa kupitia tundu lililotobolewa ukutani, sehemu ya sebuleni.

 

Alisema ilibidi watoe taarifa Polisi ambapo walifika na kuufanyia uchunguzi mwili huo na kubaini kuchinjwa kwa kutenganishwa kichwa na kiwiliwili na hata walipokitafuta, kichwa hakikupatikana, pia mtuhumiwa hakupatikana.

 

Uchunguzi ulionesha siku za hivi karibuni, mtuhumiwa huyo alikuwa na dalili za kuchanganyikiwa kiakili kwani mara kadhaa alikuwa akivua nguo na kutembea na panga muda wote.

Polisi baada ya kukamilisha uchunguzi wa awali, waliukabidhi mwili wa marehemu kwa ajili ya mazishi.

Kwa upande wa kaka wa marehemu, Aaron Yusuph Mwakatumbula ambaye pia ni msemaji wa familia, alisema baada ya kukabidhiwa mwili, waliridhia kumzika marehemu bila ya kichwa kwa kuwa walikitafuta bila mafanikio.

 

“Kiukweli kifo cha dada yangu kimeniuma sana na hivyo bado tunaendelea kumtafuta mtuhumiwa na kichwa cha marehemu kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya,” alisema Aaron.

 

Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, SACP Ulrich Matei alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema Eliakim alitenda unyama huo Aprili 23, mwaka huu saa kumi na moja alfajiri kwa kutumia kitu chenye ncha kali kumkata bibi yake shingo kwa kumtenganisha kichwa na kiwiliwili kisha kuondoka na kichwa.

 

Habari ziliendelea kueleza kuwa, kabla ya kukutwa na umauti, bibi huyo ambaye ni mzazi wa baba wa marehemu, alikuwa amelala chumbani kwake huku mtuhumiwa Eliakim akiwa amelala sebuleni ambapo alimfuata bibi yake na kutekeleza mauaji hayo.

 

Kwa upande mwingine, Kamanda Matei alitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa endapo watamuona mtu mwenye dalili za kuchanganyikiwa ili asilete madhara katika jamii.

Bado tukio hilo limeendelea kuzua utata wa mtuhumiwa huyo alipo na alikopeleka kichwa hicho huku imani za kishirikina zikihusishwa.

 

Hili ni tukio la pili la kinyama kutokea katika kijiji hicho ambapo Desemba 4, mwaka jana John Mwakalundwa aliuawa kikatili kwa kuchinjwa na mtu au watu wasiojulikana kisha mwili wake kushonwa kwenye gunia mita chache kutoka nyumbani kwake alipokuwa ametoka shambani.

STORI: EZEKIEL KAMANGA, MBEYA

Leave a Comment