×

Waziri Bashungwa Avitaka Viwanda Kutengeneza Barakoa Kwa wingi

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa (Mb).

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa (Mb) ameutaka umoja wa Viwanda vya Nguo Nchini (TEGAMAT) kuangalia uwezekano wa kuzalisha barakoa kwa wingi na kwa bei nafuu ili wananchi walio wengi waweze kumudu kununua.

 

Mhe. Bashungwa aliyasema hayo Mkoani Arusha alipotembelea Viwanda vya kuzalisha nguo vya Sunflug na A to Z ambao wameitikia wito uliotolewa na Serikali wa kuzalisha barakoa.

 

Mhe. Bashungwa amewataka (TEGAMAT) kuangalia namna Viwanda vya ndani vinavyoweza kutumia asilimia kubwa ya pamba inayozalishwa nchini. Aidha amewataka kupunguza bei ya barakoa kutoka Shillingi 1,150 kwa barakoa moja ya kitambaa kinachozalishwa kwa pamba kwa kiwango cha kati ya Shilingi 600 hadi Shilingi 800 ili itakapofika kwa mtumiaji wa mwisho isizidi Shilingi 1,500 kama kikomo cha bei.

Aidha aliwataka wenye Viwanda hivyo kuongeza uzalishaji wa barakoa kwa wingi ili ziweze kufika nchi nzima hususani vijijini kwa kuwatumia MSD wanapokuwa wanasambaza madawa Mikoani pia kusambaza barakoa zilizotengenezwa na Viwanda vyetu.

 

Katika hatua nyingine Mhe. Bashungwa alitoa onyo kwa taasisi zisizo za kiserikali zilizoomba kibali cha kuzalisha barakoa kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania kuacha mara moja kuuza barakoa hizo kwa bei ya shillingi 2,500 hadi shillingi 3,000 la sivyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Awali akitoa taarifa kwa Mhe. Bashungwa mwakilishi wa kiwanda cha Sunflug Bw. Emmanuel Mgoma alimueleza Mhe. Waziri kuwa kwa sasa kiwanda kinazalisha barakoa 25,000 kwa siku na barakoa moja inauzwa kwa Shilingi 800 kwa bei ya kiwandani.

 

Aidha, Mwakilishi wa kiwanda cha A to Z, Ndugu. Slyvester Kazi alisema kiwanda kinazalisha barakoa 15,000 kwa siku na kinauza Shilingi 1,150 kwa bei ya kiwandani. Hata hivyo Mhe. Waziri aliwataka kuzalisha kwa kiwango cha kuanzia barakoa 25,000 kwa siku.

Leave a Comment