MWILI wa aliyekuwa Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Agustino Ramadhan umeagwa leo Mei Mosi, 2020, katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, dini na siasa
Jaji Ramadhani, alifariki dunia Aprili 28, 2020, katika Hospitali ya Aga Khan, jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Jaji Ramadhan aliwahi kutumikia nafasi mbalimbali na kupata vyeo vya juu kiwemo kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Tanzania Bara na Visiwani mwaka 2002 hadi 2007, pia Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar kipindi hichohicho.
Pia ni Brigedia Jenerali ambapo alilitumikia Jeshi kabla ya kuitwa katika sekta ya Sheria na kutumikia Mahakama na kuwa Jaji Mkuu Zanzibar.
Jaji Ramadhani ni Mtanzania wa kwanza kushikilia kiti cha Urais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu tangu kuanzishwa kwa Mahakama hiyo.
Alipostaafu ujaji, alipewa kazi ya ukasisi, akatawazwa rasmi kuwa Mchungaji wa Dayosisi ya Kanisa la Anglikana lililopo Mkunazini Zanzibar na hivyo kuitwa “Mchungaji Augustino Ramadhani.” Hadi anafariki alikuwa Mchungaji wa Kanisa hilo.
Akiongea wakati wa kuaga, Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Juma, amesema kama wanataaluma wa sheria watafanya kumbukumbu ya kumuaga kitaaluma kwasababu wameshindwa kufanya hivyo sasa kutokana na janga la Corona.
Aidha ameeleza utumishi wa Jaji Ramadhani kwa taifa kama kitu cha kukumbukwa zaidi hasa alivyoweza kutumika kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo Jeshi, sheria, dini na michezo, huku akiiwakilisha nchi kwa kuwa Rais wa Mahakama ya Afrika.
