NYOTA wa Yanga, raia wa Ghana, Bernard Morrison ameibuka na kudai kuwa amekumbuka kushangilia bao la ushindi, maana kazi pekee iliyomleta nchini ni kuhakikisha anaifanikishia Yanga kupata bao.
Takriban miezi miwili sasa tangu Ligi Kuu Bara iliposimama kupisha janga la mlipuko wa Virusi vya Corona, jambo ambalo limeanza kuwachosha wachezaji wengi na baadhi yao kujikuta wakikumbuka zaidi matukio ya uwanjani ambayo kwa muda wote huu wamekuwa hawakutani nayo.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Morrison ameweka wazi kuwa pamoja na kuendelea kufanya mazoezi binafsi nyumbani kwake, kutokana na mapumziko haya ya Corona, kuna muda amekuwa akijikuta anakumbuka purukushani za uwanjani zikiwemo za kushangilia bao.
“Wakati pekee mzuri kwangu niwapo uwanjani ni pamoja na ule wa kushangilia bao tunapokuwa tumefunga, au nimefunga mimi au kumsaidia mwenzangu kwa namna yoyote ile afunge bao na mwisho wa siku litufanye kuibuka washindi.
“Hali hiyo kiukweli nimekuwa nikiikumbuka kiasi kwamba natamani ligi ianze hata leo ili mradi tu niweze kuendelea na majukumu yangu yaliyonileta hapa nchini ya kuisaidia Yanga kupata ushindi pale inapokuwa katika mchezo,” alisema Morrison
