WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi, amesema kuwa dawa za kukabiliana na virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19 ambazo Tanzania imepokea kutoka nchini Madagascar hazitogawiwa kwa wananchi kwa sasa.
Akizungumza katika hafla ya upokeaji wa dawa hizo hapa nchini, amebainisha kuwa dawa hizo zitafanyiwa utafiti kwanza na zitakapothibitika kuwa zinafaa, ndipo wananchi wataanza kutumia.
“Dawa hii tumepewa na Madagascar ili tuje tuifanyie utafiti kabla ya kuitumia. Tungekuwa tumeenda kuchukua dawa kwa ajili ya Watanzania wote tungeenda na Bombardier au Airbus, lakini tulienda na ndege ya rais,” alisema akiongeza kwamba wamepewa chupa mbili tu ambazo zitawasaidia wataalamu katika utafiti huo.
Alisema wamepewa maboksi matatu ya dawa itakayotumika kama tiba na maboksi manane ya dawa itakayotumika kama kinga, na utafiti ukikamilika zitagawiwa kwa Watanzania.
Naye Mganga Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Prof. Abel Makubi, amebainisha kuwa katika uchunguzi utakaofanyika wataaangalia kama dawa hiyo ni salama na bora katika kupambana na virusi vya corona.
Ameongeza kuwa Madagascar tayari wamefanya uchunguzi na kujiridhisha kuwa dawa hiyo inafaa ndiyo maana wameanza kuitumia.
