×

Mwandishi Kiwia Kortini kwa Tuhuma Za Uhujumu Uchumi, Utekaji – Video

 

Serikali imemfikisha Mahakamani Mwandishi wa Habari wa Gazeti la Jamhuri, Angellah Kiwia (41) na mwenzake wakituhumiwa kwa mashtaka manne, yakiwemo ya utekaji nyara na kuendesha kikosi cha uhalifu chenye silaha kilichokuwa kikijitambulisha kama Askari kanzu.

 

Angellah na Mohamed Rushaka (36), wamefikishwa jana katika Mahakama ya Kisutu ambapo katika shtaka la kwanza, wanadaiwa kati ya Machi 01 na Machi 31, 2020 kwa makusudi waliongoza genge la uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.

 

Katika shtaka la pili, washtakiwa wanadaiwa siku hiyo katika Jiji la Dar es Salaam, walimteka Seleman Mohamed wakiwa na lengo la kumpeleka katika hatari ya kumuumiza.

 

Aidha, katika shtaka lingine, washtakiwa wanadaiwa wakiwa na lengo la kulipwa, walidai Tsh. Milioni 30 kutoka kwa Seleman Mohamed, huku wakimtishia kumuua.

 

Katika shtaka la mwisho la kutakatisha fedha, wanadaiwa katika kipindi hicho walijipatia Tsh. Milioni 30 kutoka kwa Mohamed, huku wakijua kuwa fedha hizo ni zao la makosa tangulizi ya kuratibu genge la uhalifu.

 

Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka hawakutakiwa kujibu chochote huku upande wa Serikali ukisema upelelezi bado unaendelea.

 

Hakimu Chaungu aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 25, 2020 itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana.

 

Leave a Comment