×

Vodacom yawapongeza Watoa huduma wanaowasaidia wagonjwa wenye COVID-19


Taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation leo imekabidhi vyakula na vitu vingine vyenye thamani ya TZS milioni 177 kusaidia vituo vya karantini katika kupambana na kusambaa kwa COVID-19.

 


Akikabidhi msaada huo jijini Dar es salaam, Mkuu wa Idara ya Uhusiano na Mawasiliano Bi, Jacquiline Materu amesema msaada huu wa chakula umelenga watoa huduma walioko mstari wa mbele katika sekta ya afya, hususani wauguzi na pia wagonjwa walioko katika vituo vya karantini wakati wauguzi wakiwa wanawahudumia wagonjwa na wakati wagonjwa wakiwa katika vituo hivi kwa ajili ya matibabu.

 


“Leo tunajivunia wauguzi wetu ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia wagonjwa hususani katika nyakati hizi, wakihatarisha maisha yao kila siku wakati wakiwa wanawahudumia wagonjwa ambao wameathiriwa na COVID-19. Ni matumaini yetu kwamba msaada huu wa miezi miwili utakidhi baadhi ya mahitaji ya vituo hivi.” Alisema Materu.


Akipokea msaada huo Mkuu wa Utumishi wa Umma na Utawala katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, bwana Lawrence Malangwa ameishukuru Vodacom kwa msaada huo na kutoa wito kwa mashirika mengine kuiga mfano huo kwa kusaidia serikali katika kupambana dhidi ya kusambaa kwa COVID-19.

 


Vile vile katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa jijini Dar es Salaam alikuwepo Katibu wa Afya, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Sister Mathew na Mganga Mkuu wa Mkoa (RMO) wa Dar es salaam, Dr. Rashid Mfaume.

Leave a Comment