
MADIWANI wanane wa kata nane za wilayani Tunduru na kada maarufu ajulikanaye kama ‘Kiosa Kiosa’ wameachana na Chama Cha Wananchi (CUF) na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) asubuhi ya leo Mei 16, 2020.
Madiwani hao wote wamepokelewa na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho, na viongozi mbalimbali wa mkoa na wilaya.
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro, ambaye ni mjumbe wa kamati ya siasa ya wilaya ya Tunduru, amethibitisha taarifa hizo.
Madiwani hao wanatokea kata za Majengo, Nalasi Magharibi, Nandembo, Mlingoti Mashariki, Ligunga, Tinginya na Nakapanya.

Wakizungumza mbele ya Mwisho, madiwani hao wamesema kuwa wamefanya uamuzi huo kwa sababu wanahitaji chama imara kitakachowasaidia kutumikia wananchi kwa utulivu na mienendo inayooeleweka.
Madiwani hao wamefanya maamuzi hayo ikiwa ni miezi michache toka CUF kigawanyike na baadhi ya makada maarufu kuhamia ACT Wazalendo na CCM.
Na: Idd Mohamed,
Tunduru,
J’mosi, 16 Mei 2020.