×

Huu ni Mwezi wa Kusamehewa Dhambi

 

SIFA zote njema anastahiki Mola Azzawajalla, mwenye kuneemesha neema kubwakubwa na nyingine ndogondogo. Sala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad, rahmatan lil ‘alamiyn, maswahaba wake wa tangu wema hadi siku ya Kiyaamah. Hakika Mwezi Mtukufu wa Ramadhan ni mwezi miongoni mwa miezi 12 ya mwaka mzima.

 

Ambao Allah (Subuhaanahu wa Ta’ala) ameuchagua mwezi huu na akaupa hadhi kubwa na ni mwezi wenye fadhila nyingi. Miongoni mwa fadhila za mwezi huu mtukufu ni kuwa, huu ni mwezi wa kusamehewa dhambi, ni mwezi wa subira, ni mwezi wa Kur’ani, milango ya moto hufungwa na milango ya pepo hufunguliwa na Mashaytwaan hufungwa, ni mwezi ambao una siku iliyo bora kuliko miezi elfu, nayo ni siku ya Laylatul Qadr, ni mwezi wa du’aa; kwani maombi katika mwezi huu ni yenye kujibiwa, ni mwezi wa kutoa na mengi mengine.

 

Kwa hakika ni mwezi wa ‘Ibaadah na ‘amali zake zina ujira mkubwa katika mwezi huu kuliko miezi mingine. Lakini basi, ni masikitiko makubwa kwa watu walio wengi zinawapita fadhila hizi kwa sababu ya ujinga au kwa kufuata matamanio ya nafsi zao.

 

Alisikika Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) alipokuwa msikitini kwenye Minbar aliitikia Aamiyn, Aamiyn, Aamiyn, Maswahaba wakamuuliza Ya Rasuula Allaah tumekusikia ukiitikia Aamiyn mara tatu;

 

“Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema; Alinijia Jibriyl (‘Alayhis Salaam) akaniambia ni hasara iliyoje ya mtu imemfikia Ramadhani na isiwe ni sababu ya kusamehewa dhambi yake, sema Aamiyn kisha akanambia ni hasara iliyoje ya mtu aliyewadiriki wazazi wake wawili na isiwe ni sababu ya kuingia peponi, sema Aamiyn kisha akanambia ni hasara iliyoje kwa mtu aliyesikia akitajwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kisha asimswalie, sema Aamiyn.”

 

Ukweli miongoni mwa watu walio wengi wamekosa msamaha na fadhila za mwezi huu mtukufu, wameacha mafundisho sahihi ya dini yetu ya Kiislam na makosa mengi yanafanywa na wengi wetu.

Nami nakusudia hasa kutaja baadhi ya makosa yanayofanywa na walio wengi katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani, namuomba Mola Mtukufu aniwezeshe inshaAllaah.

 

Baadhi ya makosa yafanywayo Mwezi wa Ramadhani

Miongoni mwa watu wanahifadhi swaumu zao za Ramadhani na kisimamio cha Taarawiyh na swalah za faradhi kila mwaka na ibada nyingine, lakini ibada zao wanazipeleka arijojo kwa kumshirikisha Allah Mtukufu, wanakwenda kwa waganga kupiga ramli, kuangalia bahati kwa kupitia nyota na dua zao hawazielekezi kwa Allah moja kwa moja bali wanaomba mizimu, makaburi na kuvaa hirizi wakitaraji zinawakinga na madhara na Shaytwaan, hali Allah Azzawajalla amelikemea sana jambo hilo. Amesema Allah (Subuhaanahu wa Ta’ala);

 

Kama ukimshirikisha (Allah) bila shaka amali zako zitaruka patupu, (hutazipatia thawabu japo ni amali njema) na lazima utakuwa miongoni mwa wenye hasara.

Hivyo basi, mshirikina hatakubaliwa matendo yake mpaka aache ushirikina atubie kwa Mola wake na ampwekeshe katika ibada zake ndiyo zitapokelewa amali zake.

 

Na miongoni mwa watu wameufanya Mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa kucheza na mambo ya upuuzi, mwezi wa kupoteza wakati na kuifanya,

Swaumu ni jambo jepesi bila mazingatio yoyote; utawaona watu mchana wa Ramadhani na usiku wake wanacheza karata, bao na mfano wake.

 

Wamejikusanya makundimakundi wake kwa waume watoto kwa wazee wamechanganyika wala hawaoni haya na wengine wameufanya ni mwezi wa kupiga ngoma hasa ukiangalia katika nchi zetu za Afrika Mashariki; wanadai kupiga ngoma kuamsha watu kula daku na wengine hucheza ngoma hizo khasa ikaribiapo siku ya Iddi huanza kupiga ngoma zao mchana wa Ramadhani wakiomba Iddi toa, yaani wapewe pesa na huku wanaume wakiwa wamejivisha mavazi ya kike na kukata viuno hadharani! Hawajui kuwa hiyo ni laana!

Na Sheikh Ahmed Kandauma

Simu: 0673 828749 / 0746839083

Leave a Comment