×

Mavunde: Serikali Haiwezi Kuajiri Kila Mtu – Video

 

NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde, amesema wapo vijana wengi wenye sifa za kufanya kazi katika nyanja mbalimbali lakini hawana ajira kwa sababu waajiri wakubwa ni Serikali na sekta binafsi pekee ambapo licha ya kila mwaka Serikali kuajiri watumishi wapya lakini haina uwezo wa kuajiri nguvu-kazi yote iliyoko mtaani.

 

Mavunde ambaye pia ni Mbunge wa Dodoma Mjini kupitia CCM, amesema hayo leo wakati akizungumza katika mahojiano maalum na kipindi cha Front page cha +255 Global Radio na kuongeza kuwa Serikali kupitia wizara hiyo imekuwa ikiendesha program mbalimbali za kuwatengenezea ujuzi vijana na kuwawezesha ili wajiajiri na kuajiri wengine, hivyo kupunguza changamoto ya ajira na kuendesha maisha yao.

 

“Si kweli kwamba kila mmoja anaweza kuajiriwa Serikalini ama kwenye mfumo rasmi wa sekta binafsi, Serikali inaajiri kila mwaka lakini haiwezi kuajiri nguvu-kazi yote hata sekta binafsi pia. Serikali inafanya jitihada za kuwaelimisha vijana kujiajiri.

 

“Wizara yetu inao mpango wa kuwatengenezea ujuzi vijana, kutengeneza vitu mbalimbali, wapo vijana Mabibo Dar, wanatengeneza jeans, Msamvu Morogoro, wanatengeneza vifaa vya michezo, DIT Kampasi ya Mwanza pia, wote hawa Serikali inagharamia mafunzo hayo.

 

“Maamuzi ya Rais Magufuli kuhamishia makao makuu ya nchi kuwa Dodoma yameleta tija kubwa kwa wananchi wa Dodoma na nchi nzima, tumeona wafanyabiashara wengi wadogo-wadogo wakitoka maeneo mengine kuja hapa kufanya biashara zao, zamani tulizoea Dar pekee.

 

“Nilichojifunza katika kipindi hiki cha uongozi wa Rais Magufuli, ‘ni utumishi kwa watu’, sisi tuliopewa dhamana lazima tutatue changamoto za wananchi wetu, tuwahudumie na kugusa maisha yao. Hii imetusaidia sana hasa sisi viongozi vijana,” amesema Anthony Mavunde.

 

Leave a Comment