
Kifo cha George Floyd (46) kilichotokea Mei 25 huko Minneapolis nchini Marekani, kimesababisha ghadhabu kote nchini humo na baadhi ya nchi duniani, huku maandamano ya hasira dhidi ya tukio hilo yakiendelea kushamiri.
Floyd raia mweusi wa Marekani, alipoteza maisha kutokana na ukosefu wa hewa safi ya oksijeni, kwa mujibu wa uchunguzi wa madaktari wa familia yake.
Alifariki kwa kukandamizwa kwa goti shingoni na mgongoni na maafisa wa polisi wa Minneapolis, uchunguzi wa kimatibabu uliosimamiwa na familia ya Floyd umebaini hilo.
Matokeo hayo yanatofautiana na matokeo ya uchunguzi wa mwili wake uliofanywa na madktari wa kaunti ya Hennepin.
Kulingana na matokeo hayo, hakukupatikana ushahidi wowote unaohusisha ukosefu wa hewa wala kunyongwa.
Matokeo ya uchunguzi huo wa kimatibabu, pia yalibaini kwamba matatizo ya afya yalichangia pakubwa kifo cha Floyd.
Lakini madaktari waliosimamiwa na familia ya Floyd walibaini kwamba kifo chake kilikuwa ni mauaji, taarifa kutoka kwa timu yake ya sheria inasema.

“Sababu ya kifo kwa maoni yangu, kimesababishwa na ukosefu wa hewa, kutokana na kukandamizwa shingoni ambako kunaweza kukatiza oksijeni inayokwenda kwenye ubongo – na kupelekea mkandamizo mgongoni, ambako kuna tatiza upumuaji,” alisema Dk. Michael Baden, aliyekuwa daktari wa mji wa New York.
Video inayoonesha ofisa wa polisi Mzungu akiendelea kupiga goti juu ya shingo ya Floyd hata baada ya kusema kwamba anashindwa kupumua, imesababisha hasira na ghadhabu miongoni mwa raia tangu ilipoonekana wiki moja iliyopita.
Tukio hilo limesababisha maandamano ya siku nane mfululizo kote Marekani na machafuko ambayo hayajawahi kushuhudiwa kwa miongo kadhaa katika maeneo mbalimbali nchini humo.
Benjamin Crump, wakili wa familia Floyd, Juni mosi mwaka huu amesema; ”Bila shaka leo hii angekuwa hai ikiwa asingekumbana na shinikizo ya namna ile kwenye shingo yake kuliko kusababishwa na Derek Chauvin aliyekuwa afisa wa polisi pamoja na mvutano uliotokea kutoka kwa maafisa wengine wawili.”
Dk. Baden anasema, hakuwa na tatizo jingine lolote la afya ambalo huenda lingesababisha au kuchangia kutokea kwa kifo chake.

Matokeo ya uchunguzi huo yanatofautiana na yale ya uchunguzi wa awali yaliyojumuishwa kwenye malalamiko ya uhalifu dhidi ya Chauvin, ambaye ameshtakiwa kwa mauaji ya kiwango cha tatu na kuua bila kukusudia.
Utafiti wa matibabu ulisema katika ripoti hiyo kwamba, Floyd alikuwa na matatizo ya moyo na kusema kuwa yote hayo yakijumuishwa pamoja, yalikuwa na uwezo wa kutatiza mfumo wake na shinikizo kutoka kwa maafisa, huenda kulisababisha kifo chake.
Matokeo kamili ya uchunguzi wa kifo chake, bado hayajatolewa na ofisi ya matibabu ya kaunti ya Hennepin. Inasema kuwa inasubiri matokeo zaidi kutoka katika maabara.
Familia ya Floyd na wawili wao inasema mashtaka dhidi ya Chauvin yanastahili kuongezwa hadi kiwango cha kwanza cha mauaji.
Wanasema uchunguzi binafsi wa maiti yake unathibitisha kwamba maafisa wengine wawili waliochukua video wakati raia huyo mweusi anakandamizwa shingoni kwa goti, pia nao walichangia kifo chake.
HASIRA NI ZA MAUAJI AU CORONA?
Zaidi ya miji 75 imekumbwa na maandamano kwa sababu ya kifo cha George Floyd, mitaa ikiwa imefurika watu wanaoandamana bega kwa bega siku chache tu baada ya mitaa hiyo kuripotiwa kushuka kwa maambukizi ya virusi vya Corona.
Mbali na kwamba tukio la kuuawa kwa Floyd limesababisha hasira kwa jinsi maafisa wa polisi wanavyotekeleza mauaji dhidi ya raia weusi, na ni vitendo vya ubaguzi wa rangi, pia imeonesha dhahiri kuwa hasira dhidi ya hatua zilizochukuliwa na serikali katika mapambano ya Corona, nayo pia ni sababu.
Kwa sababu sasa wananchi wanaandamana bila kuchukua tahadhari yoyote, hakuna cha kuvaa barakoa, wala kunawa kwanza mikono kwa maji tiririka na sabuni. Kazi ni moja tu kuandamana na wengine kufanya ghasia.
Hasira hizi kwanza zimesababishwa na nadharia mbili; kwanza hali mbaya ya kiuchumi, lakini pia tamko la Rais Donald Trump lisililo na hekima dhidi ya tukio hilo.
Ni kwamba wananchi wa Marekani hasa weusi ndio walioathiriwa pakubwa na maambukizi ya Corona ambayo hadi jana zaidi ya watu 106,927 wamefariki huku milioni 1.8 wakiambukizwa virusi hivyo.
Hata hivyo, kitendo cha Marekani kuweka zuio la raia wake kukaa ndani katika kipindi hiki cha Corona na kuwaahidi kuwapatia fedha za kujikimu kila familia, ipo miji ambayo fedha hizo hawajapatiwa hadi sasa, hivyo tukio hili la mauaji limeamsha hasira za waliokosa fedha hizo hivyo kuona ndio njia sahihi ya kuonesha hasira zao.
Kwa sababu afya ya mwanadamu huendana na hali ya kiuchumi, hata Shirika la Afya Duniani (WHO), limetanabaisha kabisa kwamba kama kutokuwa na fedha za kujikimu ni sawa na kukumbwa na mdororo wa kiafya.
Mbali na hayo, kete nyingine ni suala la uchaguzi mkuu Novemba mwaka huu. Tayari hili Trump ameliona na kuanza kulitolea macho kwa kuonya kuwa hasira za maandamano haya zinachochewa na wanasiasa ambao wanalenga kuiangusha serikali yake.
Katika Ikulu ya Marekani kwenye Bustani ya Rose Juni mosi jioni, Trump alisema raia wote wa Marekani wameshtushwa na kifo cha George Floyd, lakini kumbukumbu hiyo haistahili kuondolewa na raia wenye ghadhabu.
“Napeleka maelfu na maelfu ya wanajeshi wenye silaha, maafisa wa jeshi na maafisa wa utekelezaji sheria kusitisha uporaji, ghasia, mashambulizi na uharibifu wa mali unaoendelea,” alisema.
Trump pia aliongeza kwamba: ”Ikiwa mji au jimbo litakataa kuchukua hatua stahiki… nitapeleka jeshi na kutatua tatizo hilo tena kwa haraka.”
“Nataka wanaopanga ugaidi huu watambue kwamba mtakabiliana na makosa kadhaa ya uhalifu,” aliongeza.
Matamshi yake yalikosolewa na mwanachama mwandamizi wa Democrats, Joe Biden, ambaye huenda akapeperusha bendera ya chama hicho katika kinyang’anyiro cha urais, na kusema Bwana Trump anatumia jeshi la Marekani dhidi ya raia wa Marekani.
Kiongozi wa walio wachache katika bunge la Seneti Chuck Schumer alisema: “Rais huyu anaweza kujidunisha kiasi gani?… Matendo yake yanaonesha uhalisia wake.”
MAUAJI YA WAMAREKANI WEUSI
Mauaji hayo yanafuatia yale ya Michael Brown huko Ferguson, Eric Garner, New York na wengine ambako kumepelekea kuanzishwa kwa vuguvugu la ‘Maisha ya mtu mweusi pia ni muhimu’.
GABRIEL MUSHI NA MITANDAO