×

Makonda: Mwizi Akikamatwa Apigwe Kipigo Kizito

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam,  Paul Makonda, amemwelekeza Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,  Lazaro Mambosasa, kuhakikisha wanawashughulikia ipasavyo baadhi ya vijana walioanza tabia ya kupora na kuiba mali za watu,  jambo linalorudisha nyuma maendeleo.

 

Amesema operesheni maalumu ya kushughulikia vibaka hao imeanza rasmi jana ambapo amemtaka kila mzazi kuhakikisha anamchunga mwanaye kwa kuwa hakuna kibaka atakaesalimika katika msako huo.

 

Ametoa agizo hilo wakati wa ziara ya ukaguzi miradi ya maendeleo Wilaya ya Temeke iliyoenda sambamba na uzinduzi wa majengo ya madarasa 124, matundu 124 ya vyoo na madawati 7,179 kwenye Shule ya Sekondari Mbagala na shule nyingine 16 wilayani humo, jambo linalokwenda kusaidia zaidi ya wanafunzi 5,000 waliofaulu na kukosa nafasi kupata uhakika wa kuendelea na masomo.

 

Akizungumza na wakazi wa wilaya ya Temeke katika ziara yake ya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo,  amesema matukio ya wizi mdogo-mdogo wa vitu kama power windows  za magari yameongezeka jijini ambapo amemtaka Kamanda wa Polisi kuhakikisha hali inakuwa sawa.

 

“Uibe simu ya Tekno au pochi haina kitu tutakuhesabu kama mwizi wa Dreamliner, kipigo chako ni cha kimataifa. Wale mnaotaka kuonja nafasi ya ukibaka kama ni nzuri onjeni na tusilaumiane, hakuna mtu yuko tayari kuharibiwa kazi kwenye hiki kipindi cha mwisho tunachofunga mahesabu,” amesema.

 

Pia  ametembelea ujenzi wa kituo cha Afya Buza na Hospital ya Yombo Vituka yenye uwezo wa kuhudumia wagonjwa 2,000 kwa siku ambapo amesema kuongezeka kwa zahanati, vituo vya afya na hospitali vinakwenda kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.

 

Pamoja na hayo  amesema ifikapo Juni 20 ataanza ziara ya siku 10 na Kamati ya Siasa ya Mkoa kwenye kila jimbo kwa lengo la kukabidhi miradi iliyokamilika ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa vitendo.

 

Katika ziara hiyo ametembelea ujenzi mitaro yenye urefu wa km 9 wilayani humo ukiwemo mtaro mkubwa  unaojengwa eneo la Serengeti kuelekea Shule ya Sekondari Kibasila na  mradi wa uwezeshaji wa vijana kupitia 10% ya mikopo inayotolewa kwenye halmashauri ambapo ameipongeza manispaa hiyo kwa namna inavyosimamia miradi ya maendeleo.

Leave a Comment