
KOCHA Mkuu wa Yanga, Mbelgiji, Luc Eymael, ameweka wazi juu ya njia ambazo anatumia kukamilisha masuala yake ya usajili kwa ajili ya kuhakikisha anapata wachezaji wenye ubora mkubwa kwa ajili ya kukiimarisha kikosi cha timu hiyo.
Ikumbukwe kwa sasa Eymael yupo nchini Ubelgiji ambapo alienda baada ya ligi kusimama kutokana na maambukizi ya Virusi vya Corona na anatarajia kurejea nchini ndani ya siku hizi tatu.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Eymael alisema hana utaratibu wa kusajili wachezaji kupitia video za Mtandao wa YouTube kwa sababu haziamini kabisa kama ni njia ya kumpata mchezaji mzuri na badala yake anatumia watu maalum wanaosaka vipaji vya soka.
Amesema anapotumiwa video za wachezaji na wataalam hao lazima pia akaangalie data za wachezaji kwenye mtandao maalum wenye takwimu za wachezaji.
“Binafsi huwa sina utaratibu wa kusajili wachezaji kupitia video za YouTube kwa sababu huwa siziamini kabisa, na hii sio njia sahihi, lakini mara nyingi natumia wale wataalamu wanaosaka vipaji vya soka kutafuta wachezaji.
“Wanaponitumia zile video huwa naangalia kisha naenda kutazama takwimu za wale wachezaji kwenye mtandao maalum unaosaidia kutunza data za wachezaji (Transfer Market) ili nijiridhishe,” alisema Eymael na kuongeza:“Jukumu langu ni kuhakikisha napata wachezaji wazuri halafu natoa mapendekezo yangu kwenye ripoti ambayo naupatia uongozi na wao ndio wanakuwa na jukumu la kukamilisha usajili.
”Yanga imehusishwa kuwa kwenye mazungumzo na wachezaji mbalimbali wakiwemo Heritier Makambo raia wa Dr Congo, Yacouba Sogne wa Burkina Fasso na Tuisila Kisinda kutoka DR Congo
Stori na Abdulghafal Ally,Dar es Salaam