×

Maandamano Yazuka London, Polisi Wajeruhiwa Vibaya

MOTO wa maandamano yaliyopewa jina la Black Lives Matter unazidi kuwaka na sasa hali siyo shwari jijini London, Uingereza, ambako maandamano makubwa yameibuka kupinga ubaguzi wa rangi na ukatili wa polisi, kufuatia tukio la Mmarekani mweusi, George Floyd, kuuawa na polisi wa Minneapolis nchini Marekani.

 

 

Maandamano hayo yaliyoanzia katika Ubalozi wa Marekani jijini London na kuelekea Westminster, yalipamba moto baada ya waandamanaji kufika Whitehall na Downing Street ambapo walianza kufanya fujo kutokana na hasira zilizosababishwa na ubaguzi wa polisi kwa watu weusi.

 

 

Jeshi la polisi lilipoingilia kati kwa lengo la kuwatawanya waandamanaji hao, hali ilizidi kuwa mbaya ambapo walijikuta wakishushiwa mkong’oto wa nguvu na kusababisha askari nane kati yao wajeruhiwe vibaya.

 

 

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza, Priti Patel, akizungumza na Shirika la Sky News, amesema fujo zilizotokea London hazikubaliki kwa sababu zinaondoa maana nzima ya watu kuandamana kwa ajili ya kuungana na familia ya George Floyd katika kipindi hiki cha msiba na badala yake yanaonekana kuwa maandamano ya kihalifu, akasisitiza kwamba wote waliohusika kwenye vurugu hizo watawajibishwa kisheria.

 

 

Mbali na kuwafanyia fujo polisi, waandamanaji pia waliing’oa sanamu ya nguli wa biashara ya utumwa wa karne ya 17, Edward Colston na kuitupa majini katika bandari ya Bristol jijini London, walijaribu kuchoma moto bendera za Uingereza pamoja na ile ya kumbukumbu ya vita ya kwanza ya dunia, ya Cenotaph Union Jack Flag.

 

 

Kama hiyo haitoshi, waandamanaji hao, pia walijaribu kuiharibu sanamu ya heshima ya waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Winston Churchil kwa kuandika maneno yaliyoonyesha kwamba waziri mkuu huyo naye alikuwa akiunga mkono ubaguzi wa rangi na unyanyasaji wa watu weusi.

 

 

Kwa mujibu wa mashuhuda, polisi walipojaribu kuwazuia waandamanaji hayo, vurugu zilianza ambapo wengine walianza kufyatua fataki huku wakiwashambulia polisi kwa mawe na fimbo hali iliyosababisha polisi watimue mbio kuokoa maisha yao.

 

 

Katika picha zinazoendelea kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, baadhi ya askari wanaonekana wakiwa wanatimua mbio, huku wengine wakiwa wamejeruhiwa vibaya na waandamanaji wenye hasira.

 

Maandamano hayo ambayo pia Jumamosi yaliweka rekodi nchini Marekani kwa kuwakutanisha watu wengi zaidi, ni mwendelezo wa maandamano makubwa yanayoendelea nchini humo na maeneo mengine duniani, kupinga mauaji ya Mmarekani mweusi, Floyd George (46), yaliyofanywa na askari mbaguzi, Derek Chauvin aliyemkandamiza shingoni kwa kutumia goti lake, kwa zaidi ya dakika nane.

 

Waziri Mkuu wa Uingereza, Borris Johnson, amenukuliwa akisema maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi yalibadilishwa maana na kuwa unyang’anyi na vurugu, jambo ambalo kamwe haliwezi kukubalika.

 

Kupitia akaunti yake ya Twitter, Waziri Mkuu Borris aliandika: “Wananchi wanayo haki ya kuandamana kwa amani wakati wakizingatia kanuni ya social distancing lakini hawana haki ya kuwashambulia polisi.

 

“Maandamano yamebadilishwa maana na kuwa ya kihuni, jambo ambalo ni usaliti mkubwa kwa sababu ya msingi ya kupinga ubaguzi. Wote waliohusika watawajibishwa!”

London, Uingereza

Leave a Comment