×

Simba Yawapiga 3-1 KMC Uwanja wa Mo Simba Arena

KIKOSI cha Simba kimetoka nyuma na kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 katika mchezo wa kirafiki ambao walicheza Juni 8, 2020 dhidi ya KMC kwenye Uwanja wao wa mazoezi wa Mo Simba Arena.

 

Simba ambao mchezo wao huo ulikuwa wa pili kuchezwa walitanguliwa katika kipindi cha kwanza dakika ya 32 baada ya Charles Ilanfya ambaye aliiliza Yanga katika mchezo wa kirafiki waliocheza Juni 7, 2020 kuwapatia KMC bao la kuongoza.

Simba walisawazisha kupitia kwa John Bocco ambaye alimalizia pasi ya Pascal Wawa baada ya kuchongwa kona.

 

Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika mchezo huo, ulikuwa na uwiano sawa wa uchezaji kutokana na timu zote mbili kushambuliana kwa zamu huku ushindani mkubwa ukionekana katika eneo la kiungo.

Simba walionekana kumiliki zaidi kipindi cha pili baada ya mabadiliko kadhaa kufanyika na kufunga mabao mawili kupitia kwa Bocco na Ajibu aliyeingia baada ya kuumia kwa Jonas Mkude na kukimbizwa Hospitali.

Mkude aliumia katika kipindi hicho cha pili baada ya kuchezewa vibaya na kuumia bega kisha kukimbizwa Hospitalini kwa usaidizi zaidi wa kimatibabu.

Kikosi cha Simba, Aishi Manila, Haruna Shamte, Gadiel Michael, Pascal Wawa, Kennedy Juma, Jonas Mkude, Luis, Said Ndemla, John Bocco Hassan Dilunga na Shiza Kichuya.

Kikosi cha KMC, Juma Kaseja, Boniface Maganga, Ally Ramadhan, Jean Baptiste, Abdallah Mfuko, Hassan Kaparata, Abdul Hilary, Mohammed Samatta, Charles Ilanfya, Emmanuel Mvuyekule na Sadala Lipangile.

Ukumbukwe kwamba jana asubuhi Juni 8, 2020 Simba iliibuka na ushindi wa mabao 4-2 katika mchezo mwingine wa kirafiki dhidi ya Transit Camp iliyochezwa katika uwanja huo.

Leave a Comment