
Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kusini, Selemani Bungara maarufu kwa jina la Bwege ametangaza kukihama Chama Cha Wananchi Cuf na kuhamia Chama cha ACT Wazalendo mara baada ya bunge kuvunjwa hapo kesho Jumanne Juni 16 2020.
Bugala ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, Juni 15, 2020 wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam;
“Ninawatangazia rasmi kuwa likivunjwa Bunge tu mimi sio tena mwanachama wa CUF karibuni ACT Wazalendo.
“Bunge hili linaloisha kesho ni bunge dhaifu,limekuwa bunge la kupokea maagizo kutoka serikalini,” amesema mbunge huyo.
===========================================
Ifahamike kuwa, nimeitumikia nafasi ya uwakilishi wa wananchi kwa maana ya ubunge wa Kilwa Kusini kwa vipindi viwili mfululizo kupitia CUF Chama cha wananchi, hivyo sina budi kukishukuru chama changu kwa kunifikisha hapa nilipo na naahidi hapa kuwa sitokisahau kamwe katika maisha yangu yote.
Niliipenda, kuipigania na kuitetea CUF Jimboni kwangu Kilwa Kusini, majimbo mengi ya Kusini na kwingineko Tanzania kwa moyo wangu wote.
Niliipenda sana CUF kwa mapambano yake ya kupigania HAKI SAWA KWA WOTE. Ninasikitika sana kuwa CUF ya sasa imeacha mapambano hayo yaliyoijengea heshima na imani kubwa ya wananchi.
Hivyo basi, ninawatangazia rasmi Watanzania wote kuwa Bunge likimaliza muda wake nitajiunga na ACT Wazalendo.
Nimejiridhisha kuwa ACT Wazalendo ni jahazi sahihi la kupigania demokrasia, haki na maendeleo ya Watanzania.
Suleiman Bungara (Bwege), Mbunge wa Kilwa Kusini.
15 Juni 2020.