
MWANAUME mmoja mwenye miaka 28, ametupwa jela siku 14 baada ya kukamatwa akikojolea kibao cha kumbukumbu ya Ofisa wa polisi Keith Palmer,aliyeuawa katika shambulizi 2017 huko nchini Uingereza.
Marehemu Keith Palmer (48), alidungwa kisu akiwa kazini katika shambulizi la Westminster la Machi 22, 2017 na alikuwa miongoni wa watu watano waliouawa na Khalid Masood.
Jiwe la kumbukumbu lake liliwekwa eneo la Carriage Gates, Westminster – Uingereza pale ambapo Palmer aliuawa.

Aidha, Juni 13 mwaka huu, njemba huyo aliyefahamika kwa jina la Andrew Banks (28), alikuwa mmoja wa waandamanaji katika maandamano yaliyofanyika eneo la kati mwa jiji la London, na kubambwa na polisi akikojolea jiwe hilo la kumbukumbu.
Kwa mujibu wa Polisi wa Metropolitan, jamaa huyo anazuiliwa katika kituo cha Essex, kaskazini mwa London, baada ya kujisalimisha katika kituoni hapo.
Aidha, leo Juni 16 Mahakama ya mji wa Westminster umemhukumu jamaa huyo kifungo cha siku 14 gerezani kwa kosa hilo.


Baba yake njemba huyo, alieleza kushangazwa na kufedheshwa na kitendo cha kipuuzi kilichofanywa na mwanaye huyo.
Polisi walikabiliana na waandamanaji jijini London siku ya Jumamosi, Juni 13, ambao walikuwa wanapinga ubaguzi wa rangi nchini humo.
Waandamanaji kadhaa walikamatwa kwa makosa tofauti ikiwemo, kufanya vurugu, kushambulia polisi, umiliki wa silaha, kuvuruga amani, kuwa walevi na kusababisha vurugu pamoja na umiliki wa dawa za kulevya.
NA MWANDISHI WETU