
UONGOZI wa Yanga, upo kwenye harakati za mwisho za kumrejesha kikosini beki wao wa zamani, Hassan Kessy, baada ya kuzungumza naye kila kitu.
Wakati msimu wa 2017/18 ulipomalizika, Kessy aliachana na Yanga na kujiunga na Nkana FC ya Zambia, kwa mkataba wa miaka miwili ambao unamalizika mwishoni mwa msimu huu.
Chanzo makini kutoka Yanga, kimeliambia Spoti Xtra kuwa, tayari wakala wa Kessy ameshafikisha ofa ya mchezaji wake huyo klabuni hapo ili kuona dili hilo linafanyika.
“Kweli sisi kama viongozi tumeshazungumza na Kessy ambaye mkataba wake na Nkana unamalizika, yeye mwenyewe yupo tayari kurudi kikosini kwetu, hivyo tuko kwenye majadiliano ya kina ambayo yametokana na baadhi yetu kujaribu kuchunguza zaidi kabla ya kumfikishia kocha.

“Hadi sasa tunasubiri baadhi ya wajumbe wa kamati ya usajili wakubaliane na hili, ili tulipenyeze kwa kocha wetu, maana kulikuwa na madai pia ya Kessy ambayo baada ya kuona tunamuhitaji akaanza kutaka alipwe kabla ya kuingia kwenye mazungumzo mapya na hayo ndiyo tunayamalizia kwa sasa.
“Unajua wakati Kessy anaachana na sisi klabu ilikuwa katika wakati mgumu, hivyo wachezaji wengi walikuwa wakidai mishahara na fedha zao za usajili akiwemo yeye ndiyo maana hata kila alipokuwa akirejea nchini alikuwa akija klabuni kufuatilia deni hilo ambalo kimsingi tunaangalia namna ya kumlipa ingawa baadhi ya viongozi wetu wamemtaka asitumie mwanya huo kutusumbua katika usajili ujao,” kilisema chanzo hicho.
Viongozi wa Yanga walipotafutwa kuzungumzia tetesi hizo, hawakua tayari, lakini pia hata Kessy mwenyewe hakupatikana ingawa inafahamika wazi, siku za nyuma tuliwahi kuripoti kwamba Yanga wanataka kumrudisha Kessy.