×

Kapombe Kuikosa Ndanda, Apelekwa Muhimbili

BEKI kiraka wa pembeni wa Simba, Shomari Kapombe ameondolewa kwenye msafara wa timu hiyo ulioelekea mkoani Mtwara kucheza na Ndanda FC kesho katika mchezo wa Ligi Kuu Bara kutokana na majeraha ya misuli.

 

Kiraka huyo alipata majeraha hayo kwenye mchezo wa Robo Fainali ya Kombe la FA uliopigwa juzi Jumatano kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam uliomalizika kwa Simba kuifunga Azam FC mabao 2-0.

 

Kapombe alipata majeraha hayo baada ya kuchezewa vibaya na kiungo mkabaji wa Azam, Frank Domayo na kusababisha beki huyo atolewe uwanjani hapo kwa machela.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Daktari Mkuu wa timu hiyo, Yassin Gembe alisema kuwa beki huyo juzi asubuhi alifanyiwa vya kina ili kujua amepata majeraha ya aina gani na ukubwa wake.

Gembe alisema kuwa beki huyo alifanyiwa kipimo cha MRI Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar, hivyo hivi sasa uongozi unasubiria majibu ya kujua tatizo lake na majibu ya vipimo vyake itatolewa hivi karibuni.

 

Aliongeza kuwa wakati akisubiria vipimo vyake, hivi sasa anaendelea na matibabu mengine ya huduma ya kwanza aliyopewa mara baada ya kuchezewa rafu hiyo.

“Kapombe amebaki Dar akiendelea na matibabu yake baada ya kupatiwa huduma ya kwanza mara baada ya kupata majeraha hayo ya kuchezewa vibaya na Domayo.“Hivi sasa Kapombe anasubiria majibu ya vipimo vyake vya MRI alivyofanyiwa Muhimbili na kikubwa ni kutaka kujua ukubwa wa jeraha lake alilolipata.

 

“Majibu hayo huenda akayapata ndani ya siku hizi mbili, lakini akiwa anaendelea kusubiria vipimo hivyo anaendelea na matibabu madogo aliyopatiwa awali,” alisema Gembe.

Wilbert Molandi na Lunyamadzo Mlyuka

Leave a Comment