
MIONGONI mwa wakuu wa mikoa walioacha simanzi kwa wananchi waliokuwa wakiwaongoza, ni Aggrey Mwanri ‘Mzee wa Soma Hiyo’ ambaye alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora kuanzia Machi, mwaka 2016 hadi Julai 3, mwaka huu.
Mwanri ambaye amestaafu, jina lake siyo geni masikioni mwa Watanzania kutokana na ucheshi, ukali na lugha za kuchekesha alizokuwa akizitumia katika kipindi cha uongozi wake mkoani Tabora.
Dk Philemon Sengati aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Magu, Mwanza, ndiye aliyerithi mikoba ya Mwanri ambaye amezua gumzo kila kona kutokana na taarifa za kustaafu kwake.
Mwanri alikuwa mmoja wa wateule wa Rais Dk John Pombe Magufuli ambaye kwa kipindi chote, ametengeneza misemo ‘iliyokiki’ zaidi ikiambatana na matukio ambayo yaliwavunja mbavu watu alipokuwa katika utekelezaji wake wa kazi.
Mbali na kuonekana kuwa mchapakazi, pia kiongozi huyo ambaye alikuwa Mbunge wa Siha (CCM), ana kipaji kingine cha kuteka hadhira na kuwafurahisha wakati anawachoma sindano ya maagizo mazito.
MISEMO ILIYOKIKI
Katika kipindi cha uongozi wake, misemo yake Mwanri iliteka vichwa vya habari, sehemu za mikusanyiko, mitandao ya kijamii na hata kutengenezea matangazo ya matamasha makubwa pamoja na wimbo.
Mojawapo ya misemo hiyo ni “Sukuma ndani,”, “Fanya kama unajikuna”, “Engineer soma hiyo-soma kwenye ramani-ngapi hiyo” na “Tutashuka na watu wa aina hiyo, jumlajumla”. Hii ni baadhi ya misemo yenye ucheshi, lakini ilizaliwa kwenye kazi muhimu zisizo za ucheshi.
Misemo hiyo ilitokana na hotuba pamoja na ziara zake katika utekelezaji wa majukumu akiwa Mkuu wa Mkoa, kwa mfano, kampeni ya kuwakamata watu wanaowapa ujauzito wanafunzi ilibatizwa jina la ‘Sukuma ndani’, ‘Tutashuka nao jumlajumla’. Onyo kwa wanaopuuzia maagizo yake au wanaoona anafanya mzaha waliambiwa wanyooshe mkono au ‘wafanye kama wanajikuna’.
Pia Mhandisi ambaye alimhisi kuwa ni ‘janjajanja’ na huenda hakuwepo kwenye eneo la ujenzi wakati wa kazi, alimpimisha vipimo kuhakikisha kama vinaendana na vilivyo kwenye ramani. Zoezi hilo lilizaa misemo ya ‘Engineer soma hiyo’.
TABORA WATAMKUMBUKA KWA HAYA
Licha ya kwamba hotuba za Mwanri zilikuwa na ujumbe na ucheshi mwingi, kiongozi huyo aliiwezesha Tabora kuwa kwenye ‘ramani’, kwa maana kwamba kupata umaarufu na taarifa za mkoa huo kufuatiliwa.
USAFI
Usimamizi wa usafi kila siku ni jambo ambalo kiongozi huyo alilisimamia kindakindaki na kuufanya Mkoa wa Tabora kusifika.
Alianzisha utaratibu wa kuhakikisha wafanyabiashara na wananchi wote mkoani humo wanajenga tabia ya kufanya usafi katika maeneo yao kila siku badala ya kusubiri kampeni ya usafi wa mwisho wa mwezi ambayo hutekelezwa kitaifa.
UPANDAJI MITI
Kwa kuwa dunia na Tanzania kwa jumla zinaendesha kampeni kabambe ya kupanda miti ili kulinda mazingira, kwa upande wa Tabora, Mwanri alisimamia jambo hili kwa umakini mkubwa.
Mwanri alizindua kampeni ya kupanda miti zaidi ya milioni 1.5 katika maeneo mbalimbali mkoa huo, hatua ambayo ililifurahisha Bunge ambalo liliitaka Serikali kumpa tuzo ya upandaji miti.
Sanjari na upandaji miti, pia mkoa huo ulizindua kampeni ya kusaka pombe zilizopigwa marufuku kwenye vifungashio vya plastiki maarufu kama viroba.
UWAJIBIKAJI
Jambo litakalokumbukwa na watumishi wa mkoa huo, ni lile la Disemba, mwaka jana ambapo Mwanri aliagiza kuahirishwa likizo ya Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya kwa maofisa wa kilimo na maofisa wote katika kipindi cha mvua.
Kiongozi huyo aliwataka watoke waende vijijini wakawahimize wananchi kulima pamba kwa ubora unaotakiwa.
KUZUIA UBADHIRIFU
Waliokumbana na ukali wa Mwanri katika kipindi cha uongozi wake ni Kaimu Ofisa Manunuzi Wilaya ya Sikonge, Silvanus Ndilabika.
Kipindi hicho aliagiza kuwekwa ndani ofisa huyo kutokana na kuwepo kwa dalili za ufisadi katika ujenzi vituo viwili vya afya.
ELIMU
Aidha, ‘mafataki’ nao walionja joto ya jiwe baada ya Mwanri kuanzisha kampeni ya kupambana na utoro kwa wanafunzi pamoja na ndoa za utotoni.
Hapo ndipo palipoibuka msemo wa sukuma ndani, kwamba ataanza kuwasukuma ndani pia majirani wa wanafunzi wanaoona watoto hawaendi shule, lakini hawatoi taarifa.
WANANCHI WAMLILIA
Mbali na Wana-Tabora kuonesha hisia zao baada ya Mwanri kustaafu, baadhi yao wameelezea hisia zao katika mitandao ya kijamii.
Mmoja wao ni Jumane Garishi ambaye alisema ‘Mwanri unaona comment zako watu tunavyokupenda kwa kujiamini na kazi zako mkuu na machejo yako kamooooon, sukuma ndani, soma hiyo, n.k yaani ulivyokuwa hupendi masihara ya kazi na matapeli wa pesa kujifanya maengineer, lakini ulipambana nao mpaka wengine walikuwa wanajuta kupangiwa Tabora.
Naye Liku Ramadhani alisema tutamisi yale maongezi ya Mwanri yaliyojaa misemo mingi ya vijana, mzaha, kufurahisha na wakati mwingine yana ubabe ndani yake, lakini yote ilikuwa ni katika kutekeleza majukumu yake ya kazi na alifanikiwa kwa namna yake.
David Chikoti, alisema kwa hakika Agrey Mwanry, uongozi anaujua…. hongera sana mzee kwa jitihada zako katika kuijenga Tabora ulizosimamia.
KWANINI ANATUMIA STAILI YA UCHESHI?
Akihojiwa na chombo kimoja cha habari, Mwanri alisema kuwa hutumia staili hiyo ili kuteka umakini wa watu.
“Ukienda ukikuta kundi la watu limejaa hapo halafu ukaanza kuchukua makaratasi ukawasomea hotuba, lazima uwe na hakika kuwa watu wote wataondoka maana wataona wanapoteza muda wanaondoka zao,” alisema.
Alisema licha ya kwamba hatumii mitandao ya kijamii, akifika kwenye eneo la tukio huangalia aina ya watu anaozungumza nao, ndipo anatafuta lugha au staili ambayo itawafanya wamsikilize kwa umakini.
MWANRI NI NANI
Aggrey Joshua Mwanri amezaliwa Julai 17, 1955 huko Siha mkoani Kilimanjaro. Katika safari yake kiutumishi, amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha kuanzia mwaka 1997 hadi 2000.
Baadaye Mbunge wa Siha kuanzia mwaka 2000 hadi 2015 ambapo aliangushwa na Dk Godwin Molel ambaye awali alikuwa Chadema kabla ya kurejea CCM.
STORI: GABRIEL MUSHI, DAR