
KLABU ya Yanga imesema wala haiwaogopi wapinzani wao, Simba ambao watacheza nao Julai 12, katika mchezo wa Kombe la Shirikisho kwa kuwa timu hiyo ni ya kawaida tu.
Yanga na Simba zinatarajia kukutana katika mchezo huo wa hatua ya nusu fainali ya Shirikisho na hii itakuwa mara ya tatu kwa mwaka huu. Mara ya kwanza timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2, ya pili Yanga walishinda bao 1-0.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli, alisema hawatishiki na mechi hiyo na badala yake wanajipanga kuona wanafanikiwa kushinda kisha waende fainali na kulitwaa kombe hilo kwa kuwa wapinzani wao ni wa kawaida.
“Simba ni timu ya kawaida kama zilivyo timu nyingine, hivyo tunajipanga kuona tunafanikiwa kutwaa kombe hilo ili tupate nafasi ya uwakilishi kimataifa.
“Tuna kikosi kizuri cha kiushindani na vijana wapo vizuri katika kuhakikisha tunashinda mechi zetu zote zilizobakia, kikosi kinaendelea na maandalizi, kwanza kufanya vizuri katika mechi yetu dhidi ya Kagera Sugar (kesho) kisha tutafikiria mchezo huo,” alisema Bumbuli.
STORI: KHADIJA MNGWAI, DAR ES SALAAM