
NI simanzi kila kona, ndivyo unavyoweza kutafsiri kishindo cha mauaji ya watu saba katika mikoa ya Mara, Arusha, Mbeya na Shinyanga ambacho kimeacha majonzi kwa jamii ya Watanzania na maswali magumu kutokana na visa vya mauaji hayo kuwa vya ajabu.
Hatua hiyo inatokana na baadhi ya mauaji hayo kushangaza kwa kuwa ndugu wa damu ndiyo wanaodaiwa kushiriki kutoa uhai wa mwenzao kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kugombania mali.
Hayo yamejiri katika kipindi cha wiki mbili zilizopita ambapo katika tukio lililotokea huko mkoani Mbeya, lilimhusisha mama na watoto ambao wamekamatwa na polisi kwa madai ya kumuua Ally Mazinge (66) ambaye ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Wilaya ya Mbarali.
Marehemu Mazinge ambaye alikuwa mkazi wa Kijiji cha Mpakani Kata ya Ubaruku Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, aliuawa kwa kukatwa na vitu vyenye ncha kali chumbani kwake muda mfupi baada ya mkewe Chausiku kutoka nje kujisaidia usiku wa kuamkia Juni 26 mwaka huu.
Akizungumza na UWAZI, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mpakani, Francis Mayemba alisema alipata taarifa kutoka kwa mmoja wa watoto wa marehemu ambapo baada ya kuelekea eneo la tukio, alitoa taarifa polisi ambao nao walifika na kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu.
Alisema baadhi ya watoto wa marehemu; Sada Ally (30) na Ramla Idd (33) walimweleza kuwa walipigiwa simu na mama yao usiku akiwapa taarifa kuhusu kifo cha baba yao ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Ubaruku.
“Ingawa hawakuambiwa sababu za kifo, lakini walipofika waliwakuta ndugu wengine na walipoingia chumbani, walishuhudia baba yao kuuawa kwa kukatwa na vitu vyenye ncha kali,” alisema.
Aidha, baada ya polisi kufika na kuwahoji, waliwakamata mama yao Chausiku Mahamoud (50), Salma Ally (20), Jumanne Ally (28), Idd Ally (24) na Hawa Ally (22).
Hata hivyo, baada ya mahojiano Sada Ally na Ramla Idd waliachiwa ingawa simu zao bado zinashikiliwa na Polisi.
Akithibitisha tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoani Mbeya, Ulrich Matei alisema chanzo cha kifo ni kuvuja damu nyingi kutokana na majeraha kichwani yaliyosababishwa na kukatwa na vitu vyenye ncha kali.
Aidha, alisema chanzo cha mauaji ni mgogoro wa kifamilia ambapo watoto na mama yao walipanga kuuza eneo la mji kumuuzia mmiliki wa Kituo cha mafuta Ubaruku, lakini marehemu alikataa.
“Mpaka sasa tunawashikilia watu watano kwa uchunguzi zaidi na uchunguzi ukikamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani,” alisema Matei.
Mmoja wa majirani Leah Mathayo, alisema marehemu hakuwa na historia ya ugomvi na mtu, hivyo ameiomba serikali kuchukua hatua.
Naye dada wa marehemu, Salma Feruzi alisema marehemu alikuwa na majeraha manne kichwani pamoja na kooni.
Naye Ustadhi, Abukari Zuberi Ngolo Katibu wa BAKWATA Wilaya ya Mbarali, mbali na kusikitishwa na mauaji, alisema marehemu alitegemewa sana Wilayani kutokana na busara zake.
DADA WASAKWA MAUAJI YA KAKA YAO!
Wakati huohuo, Mwandishi wetu kutoka Arusha anaripoti kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa mkoani humo linawasaka wanawake wawili ambao ni ndugu (dada), Neema Malisa na Sara Malisa, wakazi wa Sinoni mkoani Arusha kwa tuhuma za mauaji ya kaka yao, Mandela Malisa.
Malisa anadaiwa kuuawa kinyama kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali mgongoni, katika tukio la hivi karibuni lililohusisha ugomvi kati yake na dada zake hao.
Ilidaiwa kwamba, ugomvi wao mkubwa ulitokana na kugombea chumba kwenye nyumba ya urithi walioachiwa na marehemu baba yao.
Kwa mujibu wa Balozi wa Nyumba Kumi wa Mtaa wa Onjavutiani Kata ya Sinoni, Praygod Mhando, tukio hilo la kusikitisha lilijiri wiki iliyopita muda wa saa 9:00 alasiri katika nyumba aliyokuwa akiishi Mandela.
Mhando alisema kuwa, watuhumiwa hao walifanikiwa kutoroka baada ya tukio hilo, hivyo wanasakwa na Polisi.
Alisema kuwa, Sara ndiye anayetuhumiwa kuchukua kipande cha chupa na kumtoboa nacho Mandela mgongoni.
Alisema kipande hicho cha chupa kilimjeruhi Mandela mgongoni na kuvuja damu ambapo alikimbizwa Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.
Hata hivyo, alisema kwa masikitiko makubwa, Mandela alifariki dunia kesho yake.
Akiendelea kusimulia mkasa huo, Mhando alisema, siku ya tukio, dada zake Mandela; Sara na Neema walifika kwenye nyumba hiyo na kuingia chumbani kwa kaka yao kisha kuanza kumhoji kwa nini analala kwenye chumba alichokuwa akilala baba yao, ndipo wakatekeleza uhalifu huo.
Kwa upande wake, mke wa marehemu Mandela; Upendo Thomas alisema, siku ya tukio, muda wa asubuhi, mumewe alipigiwa simu na dada zake hao wakimtaka aondoke kwenye chumba cha marehemu baba yao.
“Baadaye dada zake walifika nyumbani, mimi nilipishana nao mlangoni kwani nilikuwa ninakwenda maliwatoni,” alisema mke wa marehemu.
Aliongeza kuwa, Mandela aliyekuwa amelala, aliamka na kumhoji dada yake kuwa kwa nini anamdharau kiasi cha kuingia chumbani kwake bila kubisha hodi, ndipo lilipotokea la kutokea baada ya vurugu kubwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, RPC Salum Hamduni alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa, polisi wanawasaka wawili hao na uchunguzi unaendelea.
WACHIMBA MADINI 4 WAUAWA KINYAMA
Pia mkoani Shinyanga, hofu na simanzi imetanda kwa wananchi wa Kata ya Segese Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoani humo baada ya wachimba madini wanne kuuawa kinyama kwa kuchinjwa na wasiojulikana.
Katika tukio hilo, mbali na mauaji, watuhumiwa walipora Carboni za kunasia Dhahabu kisha kumjeruhi vibaya mchimbaji mwingine ambaye kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Kahama.
Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji wa Kata ya Segese, Evagisla John akizungumza juzi ofisini kwake na waandishi wa Habari, alisema kuwa Majambazi hao wanadaiwa kutekeleza unyama huo usiku wa kuamkia Juni 30, mwaka huu katika kiwanda cha kuchenjulia dhahabu kilichopo katika kijiji cha Wisolele.
Afisa mtendaji huyo wa Kata, aliwataja watu waliouawa kuwa ni; Daniel William Mapunda (25) mkazi wa Msasa Mkoani Geita ambaye ni fundi mitambo katika kiwanda hicho, na Raphael Kipeya (27) msimamizi wa mradi na mkazi wa katoro Geita.
Wengine ni Lusanjo Maiko mwamasangula (31) ambaye ni mlinzi chini ya kampuni ya Sekepa ya mjini Kahama mkazi wa Tinde pamoja na Juma Jigwasanya (42) mkazi wa mkazi wa Nundu Nyakagwe Geita ambaye naye alikuwa ni mlinzi wa kampuni hiyo.
Mtendaji huyo alimtaja aliyejeruhiwa kuwa ni Exavery Mbuya (27) mkazi wa maduka mengi mkoani Mwanza.
“Kwakweli chanzo hakijafahamika na ni tukio kama yalivyo matukio mengine ya ujambazi, tukio hili tumelipokea kwa masikitiko na ni tukio la kwanza kusisimua watu wengi,” alisema Evagisla.
Akizungumzia tukio hilo Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya ulinzi ya Sekepa, Robert Pande ambaye walinzi wake wawili wamefariki katika mauaji hayo, alisema kuwa mbali ya kuonesha masikitiko juu ya tukio hilo, alidai kuwa kwa sasa kampuni yake itajipanga upya kukabiliana na matukio ya uharifu katika maeneo yanayoonekana kuwa ni hatari zaidi.
Kwa upande wake Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, ACP Joseph Paul alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa mbali na kuthibitisha kutokea kwa mauaji hayo, hadi sasa jumla ya watu sita wanashikiliwa wakihusishwa na tukio la mauaji hayo ya kikatili.
BABA ADAIWA KUMUUA BINTI YAKE, KISA MAPENZI
Aidha, ule usemi wa ‘Hasira hasara’ umedhihirika huko mkoani Mara baada ya Mwita Kembone (42), ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Kebosongo Kata ya Kisangura wilayani Serengeti mkoani humo kusakwa na polisi kwa madai ya kumpiga binti yake hadi kumuua kwa kumtuhumu kutoroshwa na mpenzi wake alipokwenda harusini.
Tukio hilo ambalo limeacha simanzi kwa familia na wanakijiji, lilijiri Juni 26, mwaka huu, muda wa kati ya saa 8:00 na 9:00 alasiri, nyumbani kwao na kuthibitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu ambaye alisema mtuhumiwa huyo anasakwa baada ya kutokomea kusikojulikana.
Babu ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Serengeti alisema, Juni 24, mwaka huu, binti Nyamhanga Mwita (20) alikwenda kwenye harusi kwa Mgosi Samo kijijini hapo na huko ilidaiwa alipata mpenzi, wakaondoka na hakurejea kwao siku hiyo na aliporudi baba yake alijichukulia sheria mkononi na kumpiga hadi kumuua.
“Tulimkamata mama mzazi wa mtoto ili aweze kutusaidia maana alijua mkasa mzima, lakini akakaa kimya. Pia tulimkamata mwenyekiti wa kitongoji hicho kwa mahojiano maana walikuwa na taarifa ya tukio, lakini hawakutoa taarifa mapema,” alisema.
Kwa mujibu wa majirani zake, Nyamhanga aliopolewa kwenye harusi na kijana wa Kijiji cha Kisangura na kwenda naye kusikojulikana.
Hata hivyo, binti huyo alirudi kwao na kumkuta mama yake ambaye aliamua kumuadhibu.
“Kwa mila na desturi za Kikurya, mtoto wa kike kulala nje ya kwao ni kosa kubwa na ni aibu kwa familia ikizingatiwa kuwa wazazi wanategemea kupata mahari kwake.
“Mama yake alimuadhibu kiasi kisha akamuacha, wakaendelea na shughuli kwa kuwa baba yake hakuwepo,” alisema mmoja wa majirani hao.
Ilisemekana kuwa, baada ya baba yake kurejea nyumbani, naye alianza kumshambulia kwa vipigo na kwa kuwa alikuwa na hasira, alimpiga akidhani anamkomesha kumbe alikuwa akimuua mwanaye.
Baada ya kubaini kuwa bintiye amefariki dunia, alianza kutafuta visingizio ikiwemo kuwa alipigwa huko alikokuwa na kutupwa Bwawa la Manchira, hivyo akawa anasaka barua ampeleke hospitalini kwa matibabu.
Suguta Mwikwabe ni msaidizi wa mwenyekiti wa kitongoji hicho ambaye alisema, mtuhumiwa huyo alifika ofisini kwake Juni 26, mwaka huu, saa 9:00 alasiri na kumuomba barua kwa ajili ya kumpeleka binti yake hospitalini kwa madai kuwa alitoroshwa na kijana mmoja wa Kisangura na kurejea nyumbani akiwa anaumwa.
Mwikwabe alisema, alimkatalia kwa kuwa mgonjwa hahitaji barua kwenda hospitalini na hakuwa ameripoti kuwa binti yake ametoroshwa wala hizo habari za kipigo hakumwambia, hivyo alimshauri apitie Polisi wampe PF-3 ndipo ampeleke hospitalini.
“Alijieleza sana, mwisho nikamwandikia barua hiyo. Kumbe alikuwa anajua ameua, hivyo akawa anatafuta namna ya kutoroka.
“Alipoondoka ofisini kwangu, alielekea nyumbani kwake, lakini muda mfupi baadaye nikaambiwa binti huyo amefariki dunia.
“Nilifika pale nyumbani kwake, sikumkuta kumbe alikuwa ameshatoroka,” alisema.
Hata hivyo, alisema watoto wake walidai dada yao alipigwa na baba yao.
Naye Mary Nyabagaka ambaye ni mama mdogo wa marehemu, alisema dada yake alimtaarifu kutoroshwa kwa binti huyo na kurudi kwake.
“Alinipigia simu akidai mtoto wake ana hali mbaya, nimuombee nikiwa natoka kuchota maji, nikamwambia afumbe macho tuombe. Nilifanya maombi kwa mbali, lakini dakika chache aliniambia binti yake amefariki dunia,” alisema Mary na kuongeza kuwa, kilichofuata ni kufanya taratibu za mazishi na kuichia Serikali kutimiza majukumu yake.
Habari hii imeandaliwa na Ezekiel Kamanga (Mbeya), Joseph Ngilisho (Arusha) na Paul Kayanda (Shinyanga).
STORI:RICHARD BUKOS, DAR