
LILE sakata la fumanizi lililotikisa Kanda ya Kaskazini na kwenye mitandao ya kijamii kati ya Agnesi Mallya (32) aliyedai kumfumania Vena Kimaro na mumewe ambalo lilikuwa linashughulikiwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, (RC) Anna Mghwira, limekosa ufumbuzi katika ofisi ya kiongozi huyo na sasa limetinga mahakamani.
Agnesi Mallya ambaye ni mwalimu katika shule moja ya msingi iliyopo katika Manispaa ya Moshi, amefikishwa mahakamani kwa kosa la shambulio la mwili Ijumaa iliyopita mbele ya Hakimu Mkazi wa Moshi, Rehema Olambo.
Akimsomea mashitaka yake, Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS), Philbert Mashurazo alidai kwamba Mei 19 mwaka huu katika eneo la Shirimatunda, katika Manispaa ya Moshi, mshitakiwa alimshambulia Vena kwa makofi na mateke na kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili.
Mshitakiwa alipoulizwa kama anakubali shitaka hilo au la, alikana na Hakimu Olambo alimuachia kwa dhamana hadi Julai 20 atakaposomewa maelezo ya awali baada ya upande wa mashitaka kueleza kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika.
Mwalimu Agnesi anadaiwa kumshambulia Vena Kimaro kwa tuhuma za kumfumania na mumewe, kisha kurekodi video na kuirusha mitandaoni huku tukio hilo likimgusa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira ambaye aliamua kuingilia kati kusuluhisha.
Juni 4 mwaka huu, mkuu huyo wa mkoa aliwakutanisha wanawake hao pamoja na mume wa Mwalimu Agness; Vicent Mallya ofisini kwake na baadaye kuwaeleza wanahabari kuwa wamekubaliana kulimaliza suala hilo nje ya utaratibu wa kipolisi.
“Nikiwa na kamanda wa polisi Mkoa wa Kilimanjaro (RPC), leo nimesikiliza suala la wanandoa wawili hao pamoja na Vena aliyedhalilishwa na wamesema wako tayari kulimaliza jambo hili,” alisema Mghwira.
Hata hivyo, baada ya kupita siku 30 tangu wanandoa hao wakutane na mkuu wa mkoa na kamanda wa polisi wa mkoa, Agnesi amefikishwa mahakamani Ijumaa iliyopita, hali inayoonesha kwamba usuluhishi nje ya taratibu za kipolisi alizosema mkuu wa mkoa, zimeshindikana.
Diwani wa Bomambuzi katika Manispaa ya Moshi, Juma Raibu aliwahi kwenda nyumbani kwa Vena, eneo la Msaranga ambapo yeye na wasamaria wema walitoa michango kumsaidia matibabu na baadaye akapelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi kutibiwa.
Akiwa hospitalini, mkuu wa mkoa alimuagiza mganga mkuu wa hospitali hiyo kumtibu mwanamke huyo hadi apone na akamuagiza kamanda wa polisi wa mkoa kuwatafuta watuhumiwa na wote walipatikana.