
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amempokea mkuu mpya wa Wilaya ya Temeke, Godwin Gondwe, na kumpa maelekezo haya:
“Ndugu yetu Godwin Gondwe karibu Temeke, umeongezewa watu kwa hiyo umeongozewa hata changamoto, kama ulikuwa unaingia ofisini saa mbili unatakiwa kuji-stretch. Hapa utapata pia watu kutoka kwenye wilaya za karibu kutoka Pwani wakija kutibiwa na huduma nyingine muhimu.
“Hatutafutani tu, utanitafuta ukikwama, au nina maelekezo kutoka kwa viongozi wetu wakubwa au mimi nimeona kuna jambo linakwenda visivyo Temeke. Mimi siyo bosi wa kutafutana kila dakika, mwisho wa siku tutapiga majungu tu.
“Nakuomba DC Gondwe ukawatembelee wananchi kutatua kero zao, unatakiwa uelewe kila kitu kinachoendelea kwenye wilaya yako (Temeke). Uwe na mfumo wa vyanzo vingi vya kukupa taarifa. Siyo nikupigie simu kukuuliza na wewe hujui kama kuna tatizo ama sehemu fulani.
“Kuja Temeke ni kama umepanda daraja, kwa sababu Temeke ni kama mkoa, kwa wanaokuja kwenye wilaya kama hizi, mara nyingi wakiiva wanapewa ukuu wa mkoa, sitaki kutabiri lakini ikimpendeza Mungu kwa yule anayemtaka.
“Nimeshaelekeza REA ifikapo Agosti 31, 2020, kila kaya iliyopo mkoa wa Dar es Salaam iwe ya ‘tembe’ au bati la ‘mgongo wa tembo’ au aina yoyote ile ya nyumba, ilihali ni ya mkazi wa Dar, iwe imeshawekewa umeme kwa Tsh 27,000, nishati tunayo ya kutosha,” amesema Makonda.