
WINGA wa AS Vita ya DR Congo, Tuisila Kisinda anayekaribia kutua Yanga, amesema anatamani kucheza pamoja na winga, Bernard Morrison katika kikosi cha timu hiyo akiamini kuwa watatengeneza kombinesheni nzuri.
Kisinda mwenye umri wa miaka 20, inasemekana kuwa alishamalizana na uongozi wa Yanga na kinachosubiriwa kwa sasa ni kufunguliwa kwa mipaka ya DR Congo Julai 15, mwaka huu ili mchezaji huyo awasili nchini kukamilisha dili lake.
Akizungumza na Spoti Xtra, winga huyo alisema tangu wafanye mazungumzo na Yanga juu ya yeye kusajiliwa na timu hiyo, amekuwa akiifuatilia na kuwaona baadhi ya wachezaji waliomvutia akiwemo winga Bernard Morrison, Feisal Salum na Papy Tshishimbi.

“Tangu Yanga waanze kunihitaji nimekuwa nikiifuatilia timu kuwafahamu baadhi ya wachezaji, kuna wachezaji wazuri sana ambao wanajituma, nimekuwa nikivutiwa na Morrison ambaye uchezaji wake umenikosha, naamini tukicheza pamoja tutafanya vizuri.
“Tshishimbi pia ni mchezaji mzuri, yupo na David Molinga ambaye nilikuwa namfahamu alipokuwa huku Congo, lakini kuna mchezaji mwingine anaitwa Feisal, nimevutiwa naye kwa sababu anacheza kwa utulivu na yupo makini na kazi yake,” alisema Kisinda.
MARCO MZUMBE, Dar es Salaam