
LEO Jumanne kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar, wanaume 22 watavuja jasho katika msako wa pointi tatu kati ya vinara wa Ligi Kuu Bara, Yanga dhidi ya Coastal Union.
Kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, Coastal Union wakiwa wenyeji walipoteza kwa kufungwa mabao 0-2, hivyo leo itakuwa ni kisasi kwao, huku Yanga wakipambana kulinda rekodi.
Cedric Kaze, Kocha Msaidizi wa Yanga, amesema wanawaheshimu Coastal Union, hivyo wataingia uwanjani kwa tahadhari kubwa kusaka pointi tatu.
“Mechi ambayo inatuhusisha na Coastal Union huwa inakuwa ngumu, hivyo tumejipanga vizuri, tunawaheshimu wapinzani wetu, lakini kwa maaandalizi ambayo tumefanya, tunaamini tutashinda.

“Wachezaji wote wapo vizuri isipokuwa Tuisila Kisinda ana asilimia chache za kucheza kwa sababu hayupo fiti, aliamka akiwa hajiskii vizuri, mazoezi ya mwisho yataamua kama anaweza kuwa sehemu ya mchezo au la,” alisema Kaze.
Joseph Lazaro, Kocha Msaidizi wa Coastal Union, alisema wataanza kazi mbele ya Yanga.
“Unasema mechi tano hatujapata matokeo mazuri, kweli, sasa tunaanza mbele ya Yanga, wachezaji wote wapo tayari, hakuna ambaye atakosekana, mashabiki wajitokeze kwa wingi uwanjani,” alisema kocha huyo.
Mbali na mchezo huo, pia leo Jumapili Ruvu Shooting itakuwa nyumbani kusaka ushindi dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar.
Awadhi Juma, Kocha Msaidizi wa Mtibwa Sugar, alisema wanahitaji pointi tatu kama ilivyo kwa Frank Msese ambaye ni Kocha Msaidizi wa Ruvu Shooting.
Rekodi zinaonesha kwamba, katika mchezo wa mzunguko wa kwanza, Mtibwa Sugar wakiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Manungu, Morogoro, walishinda 2-1.
Kwa upande mwingine, leo Namungo itaialika Ihefu kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi. Mechi ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar, wenyeji Ihefu walifungwa 0-1.
WAANDISHI: LUNYAMADZO MLYUKA, GODLIVER BUNDALA NA DANIEL AGWEYO