RAYMOND Mwakyusa almaarufu kama Vanny Boy au Rayvanny, ni moja ya wasanii wakali Bongo Flevani kutoka kwenye lebo kali ya Wasafi Classic Baby (WCB), iliyo chini ya Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.
Umaarufu wake umetokana na kuimba nyimbo kali zilizotikisa kama; Kwetu, Natafuta Kiki, Unaibiwa, Mbeleko, I Love U, Zezeta, Vumilia, Makulusa na nyingine kibao.
Ukiachana na kutoa nyimbo kali ambazo hujizolea watazamaji lukuki kwenye kijiji cha YouTube, lakini Rayvanny anaonekana kama anabebwa na Mondi, kwa nini? Kwa sababu msanii huyu hupenda kufanya kolabo na bosi wake huyo kiasi cha kuwafanya watu kujiuliza je, Rayvanny hawezi kusimama peke yake hadi kumshirikisha bosi wake huyo?
Makala haya yanakuletea takwimu za nyimbo ambazo Rayvanny amefanya peke yake, alizoshirikiana na Mondi pamoja na nyimbo za Mondi alizomshirikisha yeye ili kupata uwiano kama kweli anabebwa na Mondi au la:
KOLABO NA MONDI
Miongoni mwa nyimbo ambazo Rayvanny amemshirikisha Mondi, ni pamoja na Tetema iliyotoka mwaka 2019, mpaka sasa imejizolea jumla ya watazamaji milioni 44 mtandaoni YouTube.
Nyimbo nyingine zilizoweza kutikisa ni pamoja na Mwanza, licha kufungiwa, lakini ilikuwa ikipendwa na kupigwa kona mbalimbali nchini na hata nje ya nchi. Hadi unafungiwa, tayari ulikuwa na views Milioni 28.5.
Pia ngoma ya Vumbi iliyotoka mwaka jana, nayo imepokelewa vizuri mtaani ingawa video yake kutotoka, licha ya kuwa hajatoa video, lakini audio yake ina views Milioni 2.1. Kwa sasa, Rayvanny kamshirikisha tena bosi wake huyo kwenye wimbo unaokwenda kwa jina la Amaboko ambao unasumbua sana kitaa kutokana na staili ya nyimbo hiyo ambayo inawaruhusu watu kucheza.
Licha ya kwamba bado hajaachia video yake, wimbo huo mpaka sasa una views 876,744 kwenye YouTube huku kile kipande cha video hiyo ya Amaboko, tayari kinashika namba 1 kwenye trending, hivyo ni dhahiri kwamba akiachia video yake, itakuwa balaa.

NYIMBO ZAKE
Baadhi ya nyimbo alizotoa peke yake ni pamoja na: I Love You iliyotoka miezi 7 iliyopita ambayo ina jumla ya watazamaji milioni 11, Mbeleko iliyotoka 2017 yenye jumla ya watazamaji milioni 12, Zezeta iliyotoka 2017 yenye jumla ya watazamaji milioni 8.2.
Natafuta Kiki iliyotoka 2016/2017 yenye jumla ya watazamaji milioni 10, Miss Buza iliyotoka mwezi wa 3 yenye jumla ya watazamaji milioni 4.7, Ex Boyfriend iliyotoka iliyotoka mwezi wa tatu yenye jumla ya watazamaji milioni 3.7.
Vumilia iliyotoka mwezi wa 4 yenye jumla ya watazamaji milioni 1.6, Makulusa iliyotoka 2018 ina jumla ya watazamaji milioni 9.2 nk.
NYIMBO ZA MONDI
Nyimbo ambazo Mondi amemshirikisha Rayvanny ni pamoja na Salome iliyotoka 2017 yenye idadi ya watazamaji milioni 32, Iyena iliyotoka 2018 ina jumla ya watazamaji milioni 24 kwenye mtandao wa YouTube.
Hivyo, kulingana na takwimu hizo, kuna asilimia nyingi zinaonesha Rayvanny anabebwa na Mondi kwa kuwa kwenye nyimbo alizofanya peke yake, hakuna hata moja iliyofanikiwa kutoboa watazamaji na kufikia milioni 44.
USHAURI WA BURE
Hivyo, ili Rayvanny awe mkubwa anapaswa kuivuka rekodi ya Tetema kwenye wimbo ambao ataufanya peke yake bila kumshirikisha Mondi.
MAKALA | AMINA SAID