
BEKI wa Yanga, Juma Abdul yupo katika hatihati ya kuivaa Simba katika mchezo wa FA watakaokutana Julai 12 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar.
Juma Abdul aliumia kifundo cha mguu wa kushoto katika mchezo dhidi ya Biashara United mkoani Mara kulikosababisha aukose mchezo dhidi ya Kagera Sugar uliopigwa juzi Jumatano.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Daktari wa Yanga, Shecky Mngazija amefunguka kuwa Juma Abdul yupo katika hatihati ya kucheza mechi ya Simba pamoja na kiungo Haruna Niyonzima kutokana na kuwa majeruhi ambapo wanaendelea na matibabu hadi sasa.

“Juma Abdul aliumia mguu wa kushoto katika mechi dhidi ya Biashara United, hivyo anaendelea na matibabu pamoja na Niyonzima ambaye naye ni majeruhi, aliumia goti la kulia na haijajulikana iwapo atacheza mechi inayofuata dhidi ya Simba kwani mchezo na Biashara hawatacheza.
“Wakipata nafuu wanatakiwa wapate muda mwingine kwa ajili ya kufanya mazoezi mepesi ndipo wawe sawa, hivyo kuwatumia inategemea na jinsi watakavyokuwa, japo ni ngumu kumtumia mchezaji akiwa ametoka majeruhi na hayupo fiti,” alisema Mngazija.
Simba na Yanga zinatarajia kuvaana Julai 12 katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA ambapo mshindi atatinga fainali kutafuta tiketi ya uwakilishi wa michuano ya kimataifa mwakani japo Simba tayari imeshaipata kwenye ligi kwa kutwaa ubingwa, hivyo inahitaji heshima na kombe.
sTORI; Khadija Mngwai,Dar es Salaam