
Rais wa FIFA, Gianni Infantino, ameomba radhi kufuatia makosa yaliyotokea katika mchakato wa kuwasilisha mpango wa kuruhusu wawekezaji binafsi kuwekeza kwenye baadhi ya mashindano ya shirikisho hilo. Hata hivyo, ameendelea kupata uungwaji mkono wa viongozi wa juu wa FIFA na ataendelea kushika wadhifa wake.
Katika kikao cha Bodi ya Menejimenti ya FIFA kilichofanyika mjini Rabat, Morocco, viongozi wa shirikisho hilo walikiri kuwa kulikuwa na dosari katika namna mpango huo ulivyoshughulikiwa, hasa kwa kushindwa kuwashirikisha ipasavyo Baraza la FIFA na vyama wanachama kabla ya kuwasilishwa.
Infantino pamoja na Katibu Mkuu wa FIFA, Mattias Grafström, walituma barua ya kuomba radhi kwa makamu wa marais wa FIFA, Baraza la FIFA na vyama wanachama 211, wakiahidi kuwa makosa kama hayo hayatatokea tena.
Licha ya msamaha huo, Bodi ya Menejimenti ya FIFA ilitoa tamko la kumthibitishia Infantino kuwa bado ina imani naye na kuendelea kumuunga mkono kama rais wa shirikisho hilo.
Mpango uliokuwa ukipingwa ulikuwa wa kuanzisha kampuni mpya ijulikanayo kama FIFA Forward Enterprise (FFE), ambayo ingeruhusu uwekezaji wa sekta binafsi katika mashindano makubwa ya FIFA, ikiwemo Kombe la Dunia la Wanaume na Wanawake.
Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) lilikuwa miongoni mwa walioukosoa mpango huo, likisema umekuwa ukiendeshwa kwa ukosefu wa uwazi na hivyo kupoteza imani kwa uongozi wa Infantino.
Wakati huohuo, FIFA imekanusha taarifa zilizodai kuwa Infantino aliiahidi Morocco kuwa mwenyeji wa fainali ya Kombe la Dunia 2030 ili kupata uungwaji mkono wa mpango huo. Shirikisho hilo limesema madai hayo si ya kweli na kwamba uamuzi kuhusu uwanja utakaocheza fainali utafanywa baadaye.