×

Simba: Aisee Yanga Wamekaa!

Ni aibu kubwa kwa Yanga baada ya jana kuchezewa soka la kitabuni na kuchapwa 4-1 na Simba katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

 

Dabi yake ya kwanza.

Bao lake la kwanza la dabi. Huyu ni Mbrazil, Gerson Fraga ambaye jana aliwanyoosha Yanga kwa kuifungia Simba bao la kwanza. Fraga alifunga bao hilo dakika ya 20, baada ya kupokea pasi ya Chama.

 

Ilitokea Chama alipiga pasi ya hatari kwa Luis Miquissone aliyeingia ndani ya boksi na kupiga shuti ambalo lilitolewa na Metacha mpira ukamfi kia Chama aliyepiga chenga mabeki wa Yanga na kumpa asisti Fraga.

Yanga ndiyo walioanza kushambulia na dakika ya tatu tu, Bernard Morrison wa Yanga aliingia kwenye boksi lakini akazuiwa na mabeki wa Simba na mpira ukaokolewa.

 

Lakini Simba waliamka na dakika ya 7 na kuanzia hapo walikuwa hawakamatiki, Luis Miquissone aliingia kwenye boksi na kupiga shuti lililotoka nje kidogo ya lango.

 

Viungo wa Simba, Miquissone na Clatous Chama walikuwa tishio kubwa kwa Yanga muda wote wa mchezo wa jana. Yanga walitota jana na hadi dakika ya 69 walikuwa hawajapiga shuti lolote kwenye lango la Simba!

 

Juma Abdul aliumia dakika ya 7 baada ya kugongana na Francis Kahata na kutoka uwanjani akakaa nje akitibiwa kwa takriban dakika tano kabla ya kurejea na kuendelea na mchezo. Clatous Chama alipiga shuti kali dakika ya 10 lakini mpira ulikwenda nje kidogo ya lango.

 

Dakika ya 15 Chama aliendelea kuwasumbua Yanga baada ya kuambaa na mpira hadi kwenye boksi lakini akauacha mpira nyuma na mabeki wakaokoa. Dakika ya 20, Gerson Fraga aliifungia Simba bao la kwanza akiwa ndani ya boksi baada ya kupokea pasi ya Chama.

 

Dakika tano baadaye Mbrazili huyo alikuwa wa moto na kupiga shuti kali lililopaa juu kidogo ya lango la Yanga. Baada ya hapo, Simba walianza kucheza soka la kitabuni kama alivyoahidi kocha wao Mbelgiji Sven Vandenbroeck katika gazeti la Championi, Jumatatu iliyopita.

 

Dakika ya 31, Bocco alipiga shuti kali akiwa ndani ya boksi ambalo lilipaa juu baada ya kupewa pasi na Chama. Bernard Morrison ambaye amekuwa na matatizo ya kimkataba na uongozi, alianza kwenye mchezo wa jana lakini hakuwa na msaada mkubwa kama ilivyotarajiwa huku akishindwa kuonyesha juhudi katika kukaba.

 

Mechi hiyo ilichezeshwa na mwamuzi Ramadhan Kayoko wa Dar es Salaam, msaidizi wake wa kwanza alikuwa ni Frank Komba wa Dar, msaidizi wa pili Kassim Mpanga wa Dar na mwamuzi wa mezani alikuwa ni Nadeem Aloyce wa Dar.

 

Mwamuzi wa ziada wa kwanza Abdallah Mwinyimkuu (Singida) na mwamuzi wa ziada wa pili Abubakar Mturo (Mtwara).

 

Mashabiki wa Simba ndio waliokuja kwa wingi uwanjani jana, ukilinganisha na wale wa Yanga. Na kweli wachezaji wao hawakuwaangusha kwani waliutawala vilivyo mchezo huo na Yanga walikuwa wakiutafuta kwa tochi.

 

Kipindi cha pili, Simba walikianza kwa kasi na Chama alikosa bao la wazi dakika ya 47 akiwa ndani ya boksi akitazamana na Metacha akapiga shuti dogo ambalo lilitolewa na Metacha na kuwa kona.

 

Dakika ya 50, Chama ambaye alikuwa mwiba katika mchezo huo, aliichachafya ngome ya Yanga na kutoa pasi kwa John Bocco ambaye aliiandikia Simba bao la pili.

Na Simba waliendelea kushambulia kwa kasi na kufunga bao la tatu dakika tatu baadaye kupitia kwa Luis Miquissone kwa kazi nzuri ya Chama aliyepiga mpira uliookolewa kwa kichwa na Tshishimbi ukamfi kia Luis aliyefunga bao la tatu. Baada ya bao la tatu, mashabiki wa Yanga walianza kutoka uwanjani.

 

Dakika ya 65, Morrison alitolewa akatoka taratibu akionekana kuwa na hasira na kupitiliza moja kwa moja vyumbani, kitendo ambacho kilitafsiriwa kama ni dharau. Na hata mwamuzi wa nne alipomfuata na kumwambia huo sio utaratibu alionekana kuziba masikio na kurusha mikono.

 

Dakika ya 70 Fei Toto alifunga bao la kufutia machozi la Yanga kwa shuti kali baada ya beki wa Simba kuzuia mpira wa faulo uliopigwa na Juma Abdul.

 

Mzamiru Yassin alifunga bao la nne la Simba dakika nane tu baada ya kuingia uwanjani kuchukua nafasi ya Gerson Fraga, alifunga baada ya Metacha kupangua pasi ya Chama.

Simba: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein, Kennedy Juma, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Luis Miquissone/ Miraji Athuman dk ya 88, Gerson Fraga/Mzamiru Yassin dk ya 80, John Bocco/Meddie Kagere dk 74, Clatous Chama na Francis Kahata/Hassan Dilunga dk ya 74.

 

Yanga: Metacha Mnata, Juma Abdul, Jaffar Mohamed, Lamine Moro, Said Makapu, Papy Tshishimbi / Kelvin Yondani dk 55, Feisal Salum, Haruna Niyonzima/Ditram Nchimbi dk 55, Deus Kaseke, David Molinga na Bernard Morrison.

SAID ALLY NA JOEL THOMAS, Dar.

Leave a Comment