SHABIKI wa Yanga, Nyambese Mwita Wambura maarufu kwa jina la Kigelegele, ameeleza alivyopata wakati mgumu kuchanganya maelfu ya kuponi za promosheni ya Shinda Gari na kuchagua mshindi mmoja ambaye hata yeye hakumjua ni nani.
Kigelegele ametoa kauli hiyo wakati wa hafla ya kumkabidhi mshindi wa gari mpya aina ya Toyota FunCargo kutoka promosheni ya #ChomokaNaGari2020 #BabaLao, Didas Marik Munishi wa jijini Dar es Salaam leo Jumatano, Julai 15, 2020, katika ofisi za Global Group zilizopo Sinza-Mori jijini Dar es Salaam.

“Mimi ni shuhuda namba moja wa promosheni ya Shinda Ndinga kuliko mtu mwingine yeyote, nakumbuka nilipoitwa kwenye droo ya kwanza nilikuwa nikichanganya kuponi zote, unachukua moja bila kujua unayemchagua ni nani.
“Kuna wakati nilichukua kuponi mbili moja kushoto na nyingine kulia, nikasema nichukue ya kulia lakini baadaye nikabadilisha maamuzi nikachukua ya kushoto. Hili ni shindano la haki na limeendeshwa kwa njia ya haki na ni ukweli mtupu, nimeshuhudia kwa macho yangu na mikono yangu.
“Nawashukuru Kampuni ya Global Publishers kwa kutukumbuka sisi wanamichezo na kuturejeshea kidogo kama zawadi wanachokipata kutokana na biashara yao ya magazeti, kwa kweli ni faraja kwetu wadau wa michezo na niwapongeze washindi wote na kuwaasa Watanzania, mashindano kama haya yakitokea tena hapa Global Publishers washiriki, unaweza kupata bahati ukashinda,” amesema.
Aidha, Msemaji wa Klabu ya Soka ya Simba, Haji Manara ametoa kiasi cha fedha Tsh 40,000 kwa shabiki huyo baada ya kuwafunga magoli 4-1 katika mchezo wa nusu fainali ya kombe la Azam Sports Federation Cup huku akitoa Tsh 10,000 kwa shabiki wa Simba.
Promosheni ya Chomoka na Ndinga ilikuwa ikiendeshwa tangu Februari. 27, 2020, kupitia magazeti bora na yanayoongoza kwa habari za michezo nchini, #Championi & #SpotiXtra.