
Baadhi ya wakazi wa kaunti ya Mombasa nchini Kenya, wamezua vurugu na kuanza kumchapa polisi mmoja kichapo cha ‘mbwa mwitu’ baada ya kuwaambia wavae barakoa vyema kama wizara ya afya ya nchi hiyo ilivyoagiza.
Kikundi hicho cha watu kilisema kuwa, polisi huyo alikuwa anawasumbua mbali na kuwaambia wavalie barakoa vyema.
Polisi huyo aliponea chupuchupu baada ya kupiga mayowe, yaliyosababisha wenzake kumsikia na kisha kuja kumsaidia kutokana na kichapo cha wakazi hao.
Kupitia kwenye ripoti iliyotolewa na Kituo cha polisi cha mjini hapo, ilielezwa kuwa polisi huyo alipatwa na majeraha ya kichwa na na sehemu mbalimbali mwilini.
“Majeruhi huyo askari, alikimbizwa katika hospitali ya Coast General Hospital na kupatiwa matibabu ambayo hadi sasa tumethibitishiwa kwamba anaendelea vizuri,” ilisema taarifa hiyo.
Muuguzi mmoja wa hospitali hiyo aliyekataa kutaja jina lake kwenye vyombo vya habari, alisema kuwa polisi huyo alipata majeraha ya kichwa, lakini anaendelea kupokea matibabu.
Hiki si kisa cha kwanza kwa polisi kukabiliana na umati wa watu waliokaidi maagizo ya wizara ya afya.
Juni 6, wakazi wa kaunti ya Kisii, walichoma kituo cha polisi cha Rioma kufuatia mauaji ya mfanyabiashara wa eneo hilo huku wakidai kuwa polisi ndiyo walitekeleza kitendo hicho.
Aidha, wataalamu wa masuala ya afya, wanatafsiri kuwa wananchi wamechoka na vitendo ambavyo polisi wanawatendea au polisi wamechoshwa na ukaidi ambao wananchi wengi wanatekeleza licha ya kupewa maagizo na wizara ya afya.
Nchi hiyo hadi kufikia Julai 13, ilikuwa na watu 10,105 walioambukizwa virusi vya Corona huku kati yao 185, wakipoteza maisha.
NA MWANDISHI WETU