×

Morrison: Simba? Mbona Fresh

STAA wa Yanga, Bernard Morrison, ameweka wazi kuwa, kama Simba watamfuata na kukubaliana nao kimaslahi basi hakuna shida atasaini tu kuichezea timu hiyo msimu ujao.

 

Yanga wamekuwa wakisisitiza kuwa, Morrison alisaini mkataba mpya wa miaka miwili utakaoisha Julai 2022 baada ya ule wa miezi sita aliosaini wakati anatua kumalizika.

 

Kwa sasa Morrison amejitoa kwenye timu baada ya kichapo cha mabao 4-1 dhidi ya Simba kwenye Kombe la Azam ambapo alitoka uwanjani baada ya kufanyiwa mabadiliko.

 

Morrison ambaye ni raia wa Ghana, bado yuko nchini akisubiri majibu yake kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhusu utata wa mkataba wake na Yanga ambao wanadai walimuongeza.

 

Mshambuliaji huyo alisema, mkataba wake na Yanga umeisha tangu Julai 15, mwaka huu na kwa sasa ni mchezaji huru ambaye anaruhusiwa kujiunga na klabu yoyote itakayomuhitaji hapa Tanzania au sehemu nyingine.

“Najua kumekuwapo na taarifa kuhusu mimi kusaini kwenye Klabu ya Simba jambo ambalo siyo kweli lakini kama watakuja kuongea na mimi na tukafikia muafaka naweza kusaini kwao.

 

“Nimepanga kufanya maamuzi ya wapi nitachezea baada ya kwenda kupata mapumziko mafupi nyumbani Ghana, kwa sasa nasubiri TFF waniite ili kusikiliza mashauri yanayonihusu na ikiwezekana waniruhusu kuondoka na kufanya taratibu hizo kupitia mtandao,” alisema Morrison.

 

YANGA: KAMA UMEMALIZA MKATABA NENDA

Aidha, katika hatua nyingine Ofisa Habari wa Yanga, Hassani Bumbuli akizungumzia sakata la Morrison baada ya kusema hana mkataba na Yanga, alisema: “Kama uongozi tunasema kuwa, kama Morrison anasema amemaliza mkataba, basi tunamruhusu aende huko anakotaka kwenda na hatutamzuia.

 

“Ruksa kwenda Simba au huko Sauzi kunakotajwa, lakini wakati akienda anapotaka kwenda akae akijua kabisa ana mkataba wa miaka miwili ya kuichezea na sisi uongozi hatutaki kuongea na yeye, kwani sisi tunazungumza na TFF pekee.”

Leave a Comment